Kuna wakati katika maisha ya kiongozi ambapo cheo hakitafutwi, bali huja kama matokeo ya imani ambayo wengine wamejenga kwake.
Ndivyo ilivyokuwa Septemba 14, 2026, katika ukumbi wa mikutano wa Makao Makuu ya Mahakama ya Tanzania, ambapo wajumbe wa Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA), Tawi la Mahakama ya Rufani, walikutana kujadili masuala mbalimbali ya chama chao na, kwa pamoja, kufanya uamuzi muhimu wa kumkabidhi Jaji Ferdinand Wambali dhamana ya kuwa Mwenyekiti mpya wa tawi hilo.
Jaji Wambali anachukua nafasi hiyo baada ya kustaafu kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa tawi hilo, Jaji Shaaban Lila. Uchaguzi huo ulisimamiwa na Mlezi wa TMJA Tawi la Mahakama ya Rufani, Mhe. Augustine Mwarija.
Lakini nyuma ya taarifa hii fupi ya uchaguzi kuna simulizi pana zaidi. Ni simulizi ya imani, utulivu, busara na uongozi.
Kwa Mwanakwetu, anayemfahamu Jaji Wambali kama Jaji mtulivu, mwenye busara na asiye na papara katika mambo yake, uamuzi wa wajumbe wa TMJA una ujumbe muhimu.
Wajumbe hawakuchagua tu Mwenyekiti. Walimchagua mtu ambaye wanaamini anaweza kubeba dhamana ya kuwa sauti na msimamizi wa masuala yao ya kitaaluma na kiutendaji ndani ya chama.
Na hapo ndipo uzito wa uamuzi huu unapopatikana.
Uongozi wa TMJA ni uongozi wa chama cha kitaaluma unaowahusisha majaji na mahakimu. Mwenyekiti wa tawi ana jukumu la kuratibu shughuli za chama, kusikiliza na kuwakilisha masuala yanayowahusu wanachama, pamoja na kusaidia kujenga mazingira yanayokuza taaluma, ustawi na maadili ya kazi.
Kwa hiyo, Jaji Wambali anaingia katika nafasi hii akiwa na dhamana mpya kutoka kwa wenzake.
Kila uongozi mpya huja na matarajio mapya. Kwa TMJA Tawi la Mahakama ya Rufani, uchaguzi wa Jaji Wambali unaweza kuwa mwanzo wa ukurasa mwingine wa uongozi—ukurasa unaoweza kuleta fikra mpya, nguvu mpya na msukumo mpya katika kushughulikia masuala ya wanachama.
Masuala hayo yanaweza kugusa mazingira ya kazi, ustawi wa majaji na mahakimu, mafunzo, maendeleo ya kitaaluma, maadili ya taaluma na mambo mengine yanayowahusu wanachama.
Uamuzi wa kumchagua Jaji Wambali ndio uliomsukuma Mwanakwetu kuandika makala haya, akiwa na wivu na gere kwa wanachama wa TMJA kwa kupata kiongozi ambaye anaonekana kuwa mahiri na mwenye sifa zinazostahili dhamana hiyo.Wivu wa Mwanakwetu ni kwa sababu kama nay eye angekuwa mwana wa mahakama basi angeonja busara za uongozi wa Jaji Wambali lakini Mwanakwetu yeye ni mwanahabari tu.
Najua viongozi wa mahakama, kwa kuwa wanakaa ndani ya kuta za mahakama, wanaweza kudhani jamii haiwafahamu. Lakini Mwanakwetu anasema:
“Tunawajua, tunawafahamu, kwa kuwa nyinyi ni ndugu zetu.”
Hivyo, dhamana aliyopewa Jaji Wambali si ya kukaa kwenye kiti cha Mwenyekiti pekee. Ni dhamana ya kuongoza kwa kusikiliza, kuwakilisha kwa busara na kujenga kwa umoja.
Mahakama ya Rufani ina nafasi muhimu katika mfumo wa utoaji haki nchini. Kwa sababu hiyo, uongozi wa chama cha kitaaluma katika ngazi hiyo nao una uzito wake.
Mwenyekiti anahitajika kuwa mtu anayeweza kuunganisha watu, kusikiliza mitazamo tofauti na kusimamia masuala ya chama kwa hekima na uwiano.
Na hapa ndipo hulka ya utulivu inayohusishwa na Jaji Wambali inapoweza kuwa mtaji mkubwa.
Uongozi si kelele. Uongozi ni uwezo wa kusikiliza, kutafakari na kuchukua hatua kwa wakati sahihi.
Kwa wale wasomaji wa Mwanakwetu watambue kuwa ni muhimu pia kutenganisha majukumu haya mawili. Jaji Wambali ataendelea kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani, na wajibu wake mkuu wa kimahakama utaendelea kuwa ule ule—kusikiliza na kuamua mashauri kwa mujibu wa sheria, ushahidi na dhamiri yake ya kimahakama.
Uenyekiti wa TMJA ni nafasi ya uongozi wa chama cha kitaaluma; si mamlaka ya kuingilia uhuru wa Jaji katika kuamua kesi.
Heshima ya mahakama inajengwa pia kwa kutambua tofauti hiyo.
Kwa hiyo, kwa Mwanakwetu, habari ya Septemba 14, 2026 si habari ya uchaguzi pekee. Ni habari ya kuaminiwa. Ni habari ya wenzako kukuangalia na kusema:
“Tunakuamini ubebe dhamana hii.”
Ni habari ya Jaji ambaye kwa miaka amejenga jina lake kupitia kazi yake, utulivu wake na namna anavyotekeleza majukumu yake, sasa kupewa jukumu jingine la kuwaongoza wenzake katika chama chao cha kitaaluma.
Jaji Ferdinand Wambali, hongera sana kwa kuaminiwa.
Dhamana hii ni kubwa, lakini naamini busara, utulivu na uzoefu ulionao vitakuwa sehemu ya nguvu yako katika kuitekeleza.Mungu akuongoze, akupe hekima, afya na nguvu katika jukumu hili jipya.
Hongera kwa TMJA kwa uchaguzi. Hongera kwa wajumbe kwa imani yao. Na zaidi ya yote, hongera Jaji Wambali kwa hatua hii mpya ya uongozi.
Kumbuka:
“Tunakuamini ubebe dhamana hii.”
Mwanakwetu
makwadeladius@gmail.com
0717 649 257
.gif)




.gif)
Post a Comment