GODORO HILI SILITAKI

 




Adeladius Makwega – MBAGALA

 

Mwanakwetu alinunua godoro kwa lengo moja tu: kulala salama na kwa raha.

Alikuwa amechoka kulala kwenye virago, mikeka na majamvi. Akaona sasa ni wakati wa kupanda chati. Akajikusuru, akatafuta fedha na hatimaye akanunua godoro bora—godoro ambalo, kwa kweli, hakuwahi kulalia maishani mwake.

 

Simulizi za kwao zinasema kuwa si babu zake, si baba zake, si wajomba zake, wala shangazi na mama zake wadogo waliowahi kulalia godoro.

Afadhali kidogo kwa upande wa mama yake. Wao walikuwa wafugaji na wakati mwingine walilala juu ya ngozi za ng’ombe zenye manyoya; angalau kulikuwa na nafuu kidogo.

 

Lakini kwa upande wa baba yake mambo yalikuwa tofauti. Wao walikuwa wakulima wa mpunga, hivyo mikeka na majamvi ndiyo yalikuwa vitanda vyao. Godoro kwao lilikuwa kama kitu cha kusimuliwa, si cha kulaliwa!

 

Ndipo Mwanakwetu akaamua kuvunja mwiko wa ukoo.

Akanunua godoro.

Lakini usifikiri ilikuwa kazi rahisi!

Kabla hajalinunua, Mwanakwetu ilibidi apige ramli. Ilibidi atambike. Ilibidi atoe sadaka. Wenyewe Wapogoro wanaita kupeta mashi. Baada ya taratibu hizo kufanyika mara kadhaa, hatimaye akafanikiwa kulipata godoro lake.

 

Na sasa, Mwanakwetu alikuwa rasmi mtu wa godoro!

Alijisikia fahari.

Alijiona ameingia kwenye maisha mapya.

Lakini kumbe...

Godoro nalo linaweza kuwa na maisha yake!

Kwa hakika, tangu aanze kulalia godoro hilo, hata miezi kumi na miwili haijafika, lakini usingizi wake umegeuka kuwa adhabu.

Mchana anahangaika na usiku halali kwa raha.

 

Akilini mwake anajiuliza:

“Kumbe ndiyo maana wazee wangu wa kikeni na kiumeni walichagua kulalia mikeka, majamvi na ngozi za wanyama kwenye vitanda vyao vya kamba? Kumbe kulalia godoro nako ni kero?”

 

Hapo ndipo maneno yakaanza kuwa mengi.

Wapo wanaolitetea godoro.

Mmoja akasema:

“Unajua sisi tumejifunza kulalia magodoro wakati wa kilimo cha mkonge. Lakini kwetu tulizoea ngozi, sufi, majani ya migomba na majani ya mpunga. Vile ukilalia havina tabu.”

 

Mwingine akamjibu:

“Nyinyi kinachowasumbua ni ushamba tu! Afadhali godoro kuliko ngozi, mikeka na majamvi.”

 

Lakini tatizo la Mwanakwetu si ukubwa wa godoro.

 

Si kwamba ni dogo.

Si kwamba ni la tano kwa tano.

Tatizo ni godoro lenyewe!

Akijilaza, godoro linabonyea upande mmoja.

Na hapo ndipo balaa linapoanzia.

Badala ya Mwanakwetu kulala kwa amani, sasa kulala kwake kumekuwa kero.

 

Anasema:

“Huwezi kulala vizuri ukiwa kama uko mlimani na unataka kuanguka. Kama kubonyea, lingebonyea godoro lote! Lakini hili linabonyea upande mmoja tu—na sehemu kubwa anayolalia yeye ndiyo imebonyea.”

 

Miezi ikasonga.

Mmoja.

Miwili.

Mitatu...

Mpaka kenda.

Kumi.

 

Na sasa dazani inakaribia!

Jirani yetu huyu anazidi kujiuliza:

“Hali hii itaendelea mpaka lini?”

Kabla hajachukua uamuzi wa mwisho, anaomba ushauri.

 

Afanye nini?

Alipasue?

Alipeleke kwa fundi?

Alitupilie mbali?

Au...

Alirudie maisha ya mababu zake—ngozi, mikeka na majamvi?

 

Hapo ndipo Mwanakwetu anaposhindwa kupata jibu.

Maana alitoka kwenye mikeka na majamvi akiamini godoro litampa usingizi wa kifahari.

Kumbe ameingia kwenye godoro na  mzigo wa maumivu!

Anasema:

“Leo kidole kinauma, kesho bega linauma, kesho kutwa shingo, na mtondogoo mkono. Je, hili godoro lina usalama kweli? Lisije likawa linaniletea matatizo makubwa zaidi!”

Mwanakwetu, upo?

Kama upo, hebu tupe jibu.

Godoro hili lifanywe nini?

Kwa sababu wewe ulilinunua ili ulale kwa raha, lakini sasa umegeuka kuwa mtumwa wa godoro lako mwenyewe!

Na hapo ndipo swali linabaki:

Je, godoro linapaswa kuwa rafiki wa usingizi au adui wa usingizi?

Mwanakwetu kwa leo anaomba aishie hapo.

Anagonja majibu haraka.

Maana kabla godoro hili halijamaliza dazani yake ya miezi, yeye tayari amechoka.Na huenda kesho akaamka na kauli moja tu:

“GODORO HILI SILITAKI!”

Nakutakia siku njema.


makwadeladius@gmail.com
0717649257

 

 

0/Post a Comment/Comments