ANAYEFIA BAHARINI HAZIKWI NCHI KAVU

 

 



Adeladius Makwega-MBAGALA

 

Mabaharia walikuwa safarini baharini ndani ya chombo chao. Wakiwa katikati ya safari, ghafla chombo hicho kilikumbwa na dhoruba kali. Mawimbi makubwa yalikifanya chombo kitoke katika njia yake na kushindwa kuelekea vizuri, huku pepo za Kaskazini na Kusini zikizidi kukisukuma huku na huko.

 

Hali hiyo ilileta balaa kubwa chomboni. Safari ambayo ilitarajiwa kuchukua usiku mmoja iligeuka kuwa safari ya siku nyingi.

 

Siku ya kwanza jua lilichomoza na kuzama, kisha siku ya pili ikapita vivyo hivyo. Siku ya tatu nayo ikapita bila mabadiliko. Hadi siku ya nne, jua liliendelea kuchomoza na kuzama huku mabaharia wakiwa bado hawajui walipo wala watafika lini.

 

Vyakula vilianza kuisha. Wakati huo, walikuwa wamebakiza dumu moja tu la maji lililokuwa kando ya nahodha wao mahiri, Uzi Bini Ksaveli.

 

Chombo hicho kilikuwa kikisafiri katika bahari yenye maji ya chumvi. Kwa mabaharia, kuwa na maji safi ilikuwa jambo la msingi sana. Kiasi cha maji walichobeba kilitegemea umbali wa safari pamoja na idadi ya mabaharia waliokuwamo chomboni.

 

Maji hayo yalitumika kwa kunywa na kupikia, huku maji mengine yakizunguka kwa wingi katika bahari yenye chumvi.

 

Kumbuka siku ya nne, maji yaliyokuwa kwenye dumu la nahodha nayo yaliisha. Hata hivyo, Nahodha Uzi Bini Ksaveli hakuwafahamisha wenzake kwamba bado alikuwa na salio la dumu moja la maji.

 

Kwa kukosa maji safi, mabaharia walianza kunywa maji ya bahari yaliyokuwa na chumvi nyingi.

 

Uzi Bini Ksaveli akawaambia:

“Jamani, sasa tunakuwa ngamia. Maana ngamia anapoanza safari ndefu hulishwa chumvi nyingi ili aweze kunywa maji mengi yasiyo na chumvi. Hii humsaidia kusafiri umbali mrefu akiwa na maji aliyokunywa tumboni. Sasa na sisi leo tumekuwa ngamia.”

 

Mabaharia waliendelea kunywa maji ya bahari kwa siku sita mfululizo tangu maji yaliyomalizika. Hali hiyo ilisababisha maji mwilini mwao kupungua zaidi, huku figo zao zikishindwa kuchuja kiasi kikubwa cha chumvi kilichoingia mwilini.

 

Siku ya siku ya tano tangu waanze kunywa maji ya chumvi, akili za mabaharia zilianza kuchanganyikiwa na ufahamu wao kupungua. Kufikia siku ya sita, baadhi yao walianza kufariki.

 

Kumbuka, mabaharia hawa walikuwa chomboni kwa jumla ya siku kumi: siku nne za kupotea njia na siku sita za kunywa maji ya chumvi.

 

Saa tano ya asubuhi ya siku ya kumi, waliona kwa mbali chombo kingine kikija upande wao. Kufikia saa kumi jioni, chombo hicho kilikuwa kimewakaribia. Mabaharia wakatoa ishara ya kuomba msaada, na chombo hicho kikawasogelea.

 

Nahodha Uzi Bini Ksaveli, ambaye alizungumza lugha tano za kimataifa pamoja na lugha tano za asili, alisimama na kuzungumza na mabaharia wa chombo hicho cha pili.

 

Nahodha wa chombo hicho, aliyefahamika kwa jina la Kuandika Bini Msaliboko, akawaambia:

 

“Kwanza, poleni kwa msiba wa ndugu zenu wanne mliokuwa nao chomboni maana nasikia harufu za maiti ambao wamefariki kutokana na kunywa maji mengi yenye chumvi. Lakini huenda kilichotokea ni kutokujua tu. Hapo mlipo, mkishusha ndoo zenu baharini, mtakuta kuna maji baridi na matamu. Kuna mkondo wa mto wa maji safi unaotoka nchi kavu na kuingia baharini.”

Nahodha Uzi Bini Ksaveli na wenzake walio hai wakapatwa na butwaa, mara moja Uzi akafanya hivyo ili kuhakikisha ukweli wa maneno hayo. Alishusha ndoo baharini.

 

Kwanza, yeye mwenyewe alikunywa maji hayo. akakutana na maji matamu.

 

Baada ya hapo, Nahodha Kuandika Bini Msaliboko, aliyekuwa nahodha wa chombo hicho cha uokozi, akasema:

“Sasa nawaombeni kwanza tuwazike ndugu zenu wanne waliofariki.”

 

Walitoa miili ya mabaharia hao wane na kuiweka pamoja. Wakati wakitafuta mikeka ya kuhifadhia miili hiyo, waligundua kuwa kulikuwa na mwili wa tano—wa mwanamke aliyekuwa katika chumba cha Nahodha Uzi Bini Ksaveli.

 

Nahodha Uzi Bini Ksaveli hapo hapo akapiga yowe na kulia kwa sauti:

 

“Mpenzi wangu, Kitukuka binti Amaniya, umefariki! Mbona unaniacha mpweke? Nitasema nini kwa ndugu zako wakati nilikutorosha tu?”

 

Mabaharia waliobaki katika chombo hicho wakashangaa na kujiuliza:

“Kwa nini Nahodha Uzi hakulia kwa misiba ya mabaharia wenzake wanne, lakini sasa analia kwa uchungu mkubwa kwa kifo cha mwanamke huyu?”

 

Mazishi yalifanyika kulingana na imani na taratibu za wahusika. Miili hiyo ilizikwa kwa kutupwa baharini, kwa kuwa kwao kulikuwa na utaratibu kwamba:

 

“Anayefia Baharini Hazikwi Nchi Kavu.”

 

Baada ya mazishi, Nahodha Kuandika Bini Msaliboko alitoa ramani na kuwaeleza walipokuwa. Aliwaonesha kwamba walikuwa wamepotea na sasa walikuwa umbali wa takribani maili 500 kutoka walikokuwa wakielekea.

 

Vyombo hivyo viwili vilikaa eneo hilo kwa siku nne zaidi ili kuwapa matibabu mabaharia na nahodha wa chombo cha kwanza. Siku ya tano ilipofika, walianza safari pamoja.

 

Safari yao ilidumu kwa siku tano hadi walipofika walikokuwa wakielekea.

 

Walipofika ufukweni, mizigo haikushushwa mara moja. Kwanza, walikwenda majumbani kwa ndugu wa watu watano waliofariki. Kisha familia ziliweka matanga kwa siku tatu.

 

Balaa kubwa zaidi lilikuwa kwa Mzee Amaniya, baba mzazi wa Kitukuka.

 

Jambo hilo lilizungumzwa kwa urefu wazee wakaamua wakapige ramli ili kujua msiba wa Kitukuka Binti Amaniya ulitokana na nini? Majibu yalikuwa haya;

“Kitukuka Binti Amaniya alikunywa maji yenye chumvi.Chumvi hii ilikuwa na madhara kwake.”

Hatimaye Uzi Bini Ksaveli akafungishwa ndoa na marehemu Kitukuka, hii ilikuwa ndoa ya aliye hai na maiti. Familia ikaendelea na matanga ya binti yao kwa siku nne, na siku ya tano ndipo chombo cha kwanza kiliposhushwa mizigo yake.

 

Baada ya hapo, uvumi ulianza kusambaa kwamba chombo hicho kilipotea kwa sababu Nahodha Uzi Bini Ksaveli alikuwa amesafiri na mwanamke huyo kwa siri ndani ya chombo.

 

Wengine walidai kuwa usalama wao uliokuwa ukitegemewa ulivurugika baada ya uwepo wa mwanamke chomboni Kitukuka Binti Amaniya. Vifo vya mabaharia wanne pamoja na kifo cha mwanamke huyo vikabaki kuwa sehemu ya siri kubwa iliyowazunguka mabaharia walionusurika.

 

Lakini swali lilibaki:

Je, Nahodha Uzi Bini Ksaveli alikuwa akificha nini kuhusu Kitukuka binti Amaniya?

 

Nahodha Uzi Bini Ksaveli alificha uwepo wa maji aliyokuwa nayo na pia alificha uhusiano wake na Kitukuka. Siri hizo zilipojitokeza, ziliibua maswali na mashaka miongoni mwa mabaharia na familia. Hii inatufundisha kwamba uwazi, ukweli na uwajibikaji ni msingi wa kuaminiana, hasa wakati wa matatizo.

 

Mafunzo mengine ni haya;


Mabaharia walikumbwa na matatizo makubwa baada ya kupotea njia na kuishiwa na maji. Hii inatufundisha kuwa katika safari yoyote ya maisha, ni muhimu kujiandaa vizuri, kutathmini hatari na kuhakikisha tunakuwa na mahitaji muhimu ya kutosha.  Nahodha Kuandika Bini Msaliboko alijua kuhusu uwepo wa mkondo wa maji safi baharini. Maarifa hayo yaliwasaidia mabaharia waliokuwa wamekata tamaa. Funzo hapa ni kwamba maarifa yana thamani kubwa, na jambo tunalolijua linaweza kuwa suluhisho la tatizo kubwa wakati wa shida.

Mwanakwetu, upo? Je simulizi hii ipewe jina gani? “Kifo cha Kitukuka Binti Amaniya au Anayefia Baharini Hazikwi Nchi Kavu.”

Chaguo kichwa kimoja kati ya hivyo lakini kumbuka Anayefia Baharini Hazikwi Nchi Kavu.

 

Nakutakia siku njema.


Barua pepe: makwadeladius@gmail.com


Simu: 0717649257

 

 

 

 

0/Post a Comment/Comments