Emakulata Msafiri
Mwanakwetukids
Kulikuwa na shule ndogo yenye wanafunzi wengi waliopenda kujifunza. Tatizo lilikuwa moja tu maktaba ilikuwa na vitabu vichache na walimu hawakuwa na vifaa vya kutosha kufundishia.
Siku moja shule ilipokea kompyuta chache na intaneti. Wanafunzi walifurahi sana lakini mwalimu aliwaambia.
"Teknolojia si kwa ajili ya kucheza pekee bali ni daraja la maarifa. Mkitumia vizuri inaweza kuwafikisha popote duniani".
Kuanzia siku hiyo wanafunzi walijifunza kutafuta taarifa kutoka vyanzo vinavyoaminika, kuandika nyaraka kwenye kompyuta, kutengeneza mawasilisho na kujifunza programu rahisi za kompyuta. Walianza pia kuhudhuria masomo ya mtandaoni yaliyokuwa yakifundishwa na walimu kutoka sehemu nyingine za nchi.
Baada ya miezi kadhaa waliona changamoto nyingine. Wakulima wa kijiji walikuwa wakipoteza mazao kwa sababu hawakupata taarifa za hali ya hewa kwa wakati.
Wanafunzi wakaamua kusaidia. Walitengeneza kikundi cha kuwafundisha wakulima jinsi ya kutumia simu janja kupata utabiri wa hali ya hewa, bei za mazao sokoni na mbinu bora za kilimo. Wakulima wengi wakaanza kuvuna mazao mengi zaidi kwa sababu walijua lini wapande na lini wavune.
Habari za kazi yao zilifika kwa viongozi wa wilaya. Shule ilialikwa kushiriki maonesho ya ubunifu. Wanafunzi waliwasilisha jinsi walivyotumia teknolojia kutatua tatizo halisi la jamii yao.
Mradi wao ulipata pongezi na shule ikapata kompyuta zaidi pamoja na vifaa vya kujifunzia sayansi na teknolojia.
Miaka ilipopita baadhi ya wanafunzi walikuja kuwa wahandisi wa programu, wengine walikuwa walimu wa TEHAMA na wengine wakaanzisha biashara za kidijitali zilizowaajiri vijana wengi.
Waliporudi kutembelea shule yao ya zamani, waliwakumbusha wanafunzi wadogo jambo moja
"Teknolojia si kitu cha kuogopa wala cha kupotezea muda. Ukiitumia kujifunza, kutatua matatizo na kuwasaidia wengine inaweza kubadilisha maisha yako na ya jamii .
emakulatemsafiri@gmail.com
0653903872


Post a Comment