TEHAMA SASA NI NDUGU WA LAZIMA.


 


Adeladius Makwega – MBAGALA

 

“Moja ya kazi kubwa za Ofisi ya Rais, kupitia Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, ni kubadilisha nyaraka tulizozipokea katika nakala ngumu na kuzihifadhi katika mfumo wa kidijitali, ili ziweze kudumu kwa muda mrefu na kuwa rahisi kuzifikia pale zitakapohitajika.”

 

Hayo yalikuwa ni miongoni mwa maneno ya ukaribisho aliyosema Mary Mollel alipokuwa akimkaribisha Mwanakwetu katika chumba kikubwa kilichojaa mitambo na vifaa mbalimbali vinavyotumika katika kazi ya kuhifadhi na kuzipa uhai wa muda mrefu nyaraka za Taifa.

 

Katika chumba hicho, Mwanakwetu alishuhudia kazi hiyo ikifanyika kwa umakini na weledi mkubwa, ikisimamiwa na watumishi wawili wa taasisi hiyo: Mary Mollel kutoka Huduma za Nyaraka, pamoja na Joseph Mnaya kutoka Kitengo cha TEHAMA.

 

Kwa Mwanakwetu, ilikuwa ni picha halisi ya namna historia ya Taifa inavyoweza kuunganishwa na teknolojia ya kisasa.

 

Akizungumzia umuhimu wa TEHAMA katika kazi hiyo, Joseph Mnaya kutoka Kitengo cha TEHAMA cha Ofisi ya Rais, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, alisema:

 

“Kwa hakika, TEHAMA imekuwa mchezaji hodari katika teknolojia ya sasa. Huwezi kufanya mambo mengi kwa ufanisi kama unaikwepa TEHAMA. Kwa sasa, TEHAMA ni ndugu wa lazima katika maendeleo.”

 

Maneno hayo yana uzito wake.

 

Dunia imebadilika. Teknolojia imeingia katika kila eneo la maisha, na hata nyaraka ambazo zamani zilihifadhiwa kwenye makaratasi pekee sasa zinahitaji kupewa maisha mapya kupitia mifumo ya kidijitali.

 

Mwanakwetu alipoendelea kufuatilia kazi hiyo, alimsikia Joseph Mnaya akimwelekeza Bi. Mollel kuhusu namna ya kuiweka nyaraka moja kabla ya kuichanganua:

 

“Hii nyaraka usiiweke ikiwa imepinda; lazima iwe imenyooka ili tuweze kuiscani vizuri.”

 

Kauli hiyo ndogo inaonyesha kwamba hata katika kazi kubwa ya kuhifadhi historia ya Taifa, umakini katika jambo dogo unaweza kuwa na maana kubwa.

Nyaraka inapohifadhiwa vibaya, inaweza kupoteza ubora wake. Lakini inapochakatwa kwa umakini na kuingizwa katika mfumo wa kidijitali, inakuwa sehemu ya hazina ambayo inaweza kuwafikia vizazi vya sasa na vijavyo.

 

Msomaji wangu, haya yote ni muhtasari wa kazi niliyoishuhudia katika Ofisi ya Rais, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, jijini Dodoma, tarehe Agosti 27, 2026, kama Mwanakwetu nilivyoona.

Ni kazi ambayo huenda kwa mtu wa kawaida ikaonekana ni ya kawaida tu—makaratasi, mashine na kompyuta.

Lakini nyuma ya kila karatasi kuna historia.Nyuma ya kila nyaraka kuna taarifa.Na nyuma ya taarifa hizo kuna kumbukumbu ya Taifa.

Ndiyo maana katika zama hizi za kidijitali, TEHAMA si anasa tena.

TEHAMA sasa ni ndugu wa lazima.

makwadeladius@gmail.com

0717649257

 

















 


 

0/Post a Comment/Comments