Emakulata Msafiri
Mwanakwetukids
Kila asubuhi watoto wengi walikusanyika kwenye kituo cha basi wakisubiri usafiri wa kwenda shule. Lakini kulikuwa na jambo la ajabu.
Kila Jumatatu kwenye benchi la kituo hicho kulikuwa na kitabu kipya cha hadithi. Hakukuwa na jina la mwenye kitabu,wala hakukuwa na mtu aliyekiona akiwekwa pale.
Watoto walikisoma huku wakisubiri basi. Baada ya kukimaliza walikirudisha pale pale.
Wiki iliyofuata kitabu kingine kilionekana. Kisha kingine baada ya miezi michache watoto wote waliokuwa wakisubiri basi walikuwa wamezoea kusoma kabla ya safari.
Siku moja Musa aliamua kufika kituoni mapema sana ili ajue siri hiyo.
Alijificha nyuma ya nguzo. Saa kumi na moja alfajiri alimuona mzee mmoja akija taratibu na begi la zamani. Alitoa kitabu akakipangusa vumbi akakiweka kwenye benchi kisha akaondoka bila kusema neno.
Musa alimfuata "Babu kwa nini unaacha vitabu hapa bila kujitambulisha?"
Mzee alitabasamu "Nilipokuwa mtoto sikuweza kwenda shule. Nilijifunza kusoma nikiwa mtu mzima. Sasa nataka watoto wengine wagundue kuwa dakika chache za kusoma kila siku zinaweza kubadilisha maisha yao."
Kuanzia siku hiyo watoto nao walianza kuleta vitabu walivyokwisha kusoma ili wengine wavisome.
Baada ya muda kituo kile cha basi hakikujulikana tu kwa kusubiri usafiri bali pia kama kituo kidogo cha maarifa.
emakulatemsafiri@gmail.com
0653903872



Post a Comment