.gif)
Adeladius Makwega
Ofisi ya Rais, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka – Dodoma.
“Unajua, suala la kuhifadhi kumbukumbu siyo suala gumu; linahitaji tu utayari wa mtu au taasisi husika. Ngoja nikwambie, mimi nimesoma Shule ya Sekondari Mwenge. Pale shuleni, tangu kitambo, kulikuwa na tabia ya kuhifadhi vizuri kumbukumbu za shule ile.”
Ndugu huyu aliendelea kusema:
“Kuna siku maalumu ambayo huwa ni Siku ya Albamu ya Shule. Wanafunzi huruhusiwa kuzitazama albamu za shule tangu ilipoanzishwa. Albamu hizo zina picha za walimu wa shule, wanafunzi wake na viongozi mbalimbali waliofika shuleni. Nakumbuka niliona picha za walimu wa zamani wakiwa wamevaa kaptula na soksi.”
Msimuliaji aliendelea kuyaburudisha masikio ya Mwanakwetu mithili ya wimbo wa Bongo fleva:
“Nakwambia, kama mtu alisoma Mwenge Sekondari, lazima picha yake ipo katika albamu ya shule. Hili linakuwa jambo jema, hasa kama mtu huyo atakuja kuwa kiongozi mkubwa baadaye, kwa sababu taarifa zake zinakuwepo hadi kwenye picha ya siku aliyoingia shuleni, matukio mbalimbali ya shuleni na hatimaye siku aliyohitimu.”
Hayo ni maelezo ya Mwalimu Lukas Masunzu, mwandishi wa vitabu nchini Tanzania, msomi wa Shahada ya Uzamili katika Elimu na mwalimu wa Shule ya Sekondari Urambo, Tabora.
Mwalimu Masunzu aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na Mwanakwetu mwanzoni mwa Agosti 2026 kwa njia ya simu.
“Hebu nikuulize, nani leo hapendi kuona taarifa zake za zamani—namna alivyokuwa mdogo na namna alivyokuwa akisoma shuleni? Taarifa zilizopo ni zile za kwenye mafaili tu. Yapo wapi maisha yake mengine nje ya mifumo rasmi? Maana yake ni kwamba hakuna kumbukumbu zilizohifadhiwa.”
Mwalimu Masunzu alimteka Mwanakwetu mithili yu chini ya ulinzi wa askari wa dola ya Rumi katika vita vya Oktavia na Kleopatra wa sita.
“Kwa nini iwe hivyo wakati wengi wetu tumeishi, tumekaa na kusoma katika maeneo mbalimbali? Watanzania hatuna utaratibu mzuri wa kuhifadhi kumbukumbu. Sasa mimi ninaona ni muhimu na ni wajibu wa mimi, wewe na yule kuanzia leo kuiga mfano wa Shule ya Sekondari Mwenge.”
Mwalimu Masunzu alihitimisha mazungumzo yake na Mwanakwetu kwa kuupiga msumari katika jeneza la kuzika uvivu wa kuhifadhi kumbukumbu na kueleza faida za kuhifadhi picha za taasisi.
“Taasisi yenye picha na kumbukumbu inaonesha safari yake ya mafanikio kwa miaka mingi iliyopita, ya sasa na hata ijayo. Picha nzuri zilizopangwa vizuri zinaonesha kwamba taasisi ipo kazini na inaaminika.
Wageni na wadau wanapofika na kuona historia ya matukio mazuri ya taasisi, wanapata imani nayo. Wanaona kwamba taasisi haijaanza leo, bali ina historia na imekuwa makini katika mambo yake.”
Mwanakwetu alipomaliza mazungumzo na Mwalimu Masunzu na kisha kuamua kuyaandaa maelezo haya ili kuendelea kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kuhifadhi kumbukumbu.
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Urithi wa picha na sauti unaotokana na matukio mbalimbali duniani uko hatarini. Hali hii inachangiwa na mambo mbalimbali, yakiwemo utunzaji duni wa kumbukumbu, maendeleo ya teknolojia na uharibifu wa makusudi.
Hali hiyo imesababisha Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kutenga siku maalumu kwa ajili ya kuelimisha umma kuhusu umuhimu wa kuhifadhi kumbukumbu za picha na sauti.
Kwa mantiki hiyo, UNESCO inatambua Oktoba 27 kuwa Siku ya Kimataifa ya Urithi wa Picha na Sauti, ikiwa ni siku ya kuwakumbusha watu, taasisi na jamii kwa ujumla umuhimu wa kuhifadhi kumbukumbu hizo kwa ajili ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Kumbukumbu si mabaki ya jana pekee, bali ni daraja linalounganisha jana, leo na kesho. Picha, sauti, nyaraka na taarifa za matukio mbalimbali ni sehemu ya utambulisho wa mtu, taasisi na taifa. Tunapozihifadhi kwa usahihi, tunawapa vizazi vijavyo nafasi ya kuijua historia yao kwa ushahidi halisi. Lakini tunapozipuuza, tunahatarisha kupoteza sehemu muhimu ya historia ambayo haiwezi kurejeshwa.
Ebu fikiria kisa cha Lukas Masunzu na shule ya Sekondari Mwenge kuwa
“Wale walimu walikuwa wakivaa kaptula na soksi.”
Hili ni jambo geni leo hii na kulingana na taratibu za utumishi wa umma kuvaa hivyo ni kosa, jamii inaweza kujifunza tu kupitia picha hiyo jambo hili la zamani kuwa sahihi lakini leo ni kosa.
Wakati ni sasa kwa kila mmoja wetu, familia, shule, taasisi na taifa kutambua kuwa kuhifadhi kumbukumbu ni wajibu, si anasa. Tusisubiri hadi historia ipotee ndipo tuanze kuitafuta. Tuanze leo kuhifadhi picha, sauti, nyaraka na matukio muhimu, kwa sababu kile tunachokihifadhi leo ndicho kitakachozungumza juu yetu kesho. Historia inaweza kusimuliwa kwa maneno, lakini kumbukumbu iliyohifadhiwa vizuri huipa historia sauti na sura.
Mwanakwetu upo? Kumbuka:
“Siku ya Albamu ya Shule.”
Nakutakia Siku Njema.
Barua pepe:
Simu: 0717649257
NB Natoa shukrani za dhati kwa Afisa Elimu Lukas Masunzo wa Shule ya Sekondari Urambo Tabora-Tanzania.





.gif)
Post a Comment