NDOA YA KIKRISTO NI AGANO LA MAISHA HADI MAUTI — ASKOFU MBILU”

 


ADELADIUS MAKWEGA — DODOMA, TANZANIA

 

 

Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Mchungaji Dkt. Msafiri Mbilu, amesema kuwa ndoa ya Kikristo ni agano la maisha ya kudumu, linalowataka wanandoa kuishi pamoja kwa uaminifu, upendo na kujitoa hadi kifo kitakapowatenganisha.

Akifungisha ndoa kati ya Francis Wambura, mtumishi katika Vyombo vya Ulinzi na Usalama, na Bi. Ruth Josephy Jally, Diwani wa Viti Maalumu wa Tarafa ya Lushoto katika Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto, Mkoa wa Tanga, Askofu Dkt. Mbilu alisema kuwa utoaji wa cheti cha ndoa mara baada ya kufungwa kwa ndoa una maana kubwa katika maisha ya wanandoa.

 

Alisema kuwa tofauti na vyeti vya elimu ambavyo hutolewa baada ya mtu kusoma kwa muda mrefu na kufikia hatua ya kuhitimu, cheti cha ndoa hutolewa mapema kwa sababu kinaashiria kuanza kwa maisha mapya ya wanandoa yanayopaswa kudumu katika safari yao yote ya maisha.

 

“Unajua kwa desturi ya dunia, vyeti huwa vinatolewa baada ya kusoma kwa muda kadhaa na kuhitimu masomo yao, tangu elimu ya awali hadi udaktari wa falsafa. Lakini katika ndoa, cheti kinatolewa mapema. Maana yake ni kwamba maisha haya ni endelevu hadi mauti.” amesema.

 

Askofu Dkt. Mbilu aliyasema hayo katika Kanisa Kuu la Uaskofu la Dayosisi ya Dodoma, wakati wa ibada ya kufungisha ndoa hiyo, akiwakumbusha wanandoa wote kwamba ndoa ya Kikristo si jambo la muda mfupi, bali ni agano linalowataka mume na mke kushikamana katika nyakati zote za maisha, katika furaha na changamoto.

 

Katika ibada hiyo, Mchungaji Veronika Kafwela, aliyesoma Neno la Mungu na kuhubiri, alitumia Kitabu cha Wimbo Ulio Bora, sura ya nne, mstari wa 7 hadi 11, kama msingi wa mahubiri yake.

Akifafanua somo hilo, Mchungaji Kafwela aliwakumbusha waumini na wanandoa umuhimu wa kujifunza kuona na kuthamini mambo mema yaliyomo ndani ya wenzi wao, badala ya kujikita katika udhaifu na mapungufu yao.

 

“Mungu anatambua madhaifu ya binadamu, lakini katika wimbo huu Mungu anayataja mazuri. Kwa hiyo, kila mmoja lazima atambue kulitazama hata zuri moja kutoka kwa mwenzake na siyo mabaya tu.” Amesema Mchungaji Kafwela.

 

Amesema kuwa msingi huo ni muhimu katika maisha ya ndoa kwa sababu wanandoa ni wanadamu wenye mapungufu, hivyo wanapaswa kujifunza kuvumiliana, kusameheana, kuheshimiana na kuendeleza upendo ambao Mungu ameuweka kati yao.

Ibada hiyo ya ndoa ilihudhuriwa na wachungaji Daniel Sangolo, Mchungaji Veronika Kafwela na Mchungaji Amoni Mponzi kutoka Dayosisi ya Dodoma, pamoja na Katibu Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Mwalimu Julius Madiga.

 

Ndoa hiyo imefungwa kwa misingi ya imani ya Kikristo, ikiwa ni mwanzo wa safari mpya ya maisha ya Francis Wambura na Ruth Josephy Jally, wakitakiwa kumweka Mungu kuwa msingi wa familia yao na kuishi kwa upendo, uaminifu, uvumilivu na hofu ya Mungu katika maisha yao yote.

Barua pepe: makwadeladius@gmail.com
Simu: 0717 649 257









 




















 

0/Post a Comment/Comments