Natafuta Siri ya Jina SALAMA

 



Adeladius Makwega

Ofisi ya Rais, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa – DODOMA

 

Mwanakwetu alipofika katika taasisi hii ya umma alibaini kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Rasilimali Watu anaitwa Salama Saidi Mohamed.

 

Akilini mwake yalimjia majina mengi miongoni mwa hayo, mathalani mwanahabari na mwanamuziki wa zamani Salama Jabir.

Huku akisema moyoni, jina SALAMA ndiyo hilo hilo SALMA, SALIMA.

 

Waswahili na wasomi wa lugha ya Kiswahili wanapuliza zumari lao la sarufi ya lugha hii wakinadi kuwa:

 

“Hoja hii inatokana na msingi wa kutobadilika kwa konsonanti za mzizi wa jina hilo, yaani S, L na M. Iwe kwa SALIMA, SALAMA, SALMA, na hili ni kwa binti/mwanamke, huku vivyo hivyo kwa mvulana/mwanaume ikiwa SALIMU.”

 

Isitoshe, jina hilo linaweza kuumbwa na irabu A, I au E, huku irabu A ikijirudia na wakati mwingine irabu I ikidondoshwa kulingana na matamshi.

 

Waswahili wa Mbagala, nduguze Mwanakwetu, wanasema:

 

“Jina hilo linaweza kuwa SALAMA, SALIMA, SALMA, SAALIMA au SELIMA/SELMA, nakadhalika. Huku jina hilo likitumiwa kama jina la kiume likitamkwa SALIM, SALIMU kama nilivyosema awali.

 

Jina hilo kwa asili linatokana na lugha ya kale ya Kiebrania, huku lugha nyingine kama Kiarabu na Kiswahili likilichukua kama lilivyo, na maana yake ni AMANI.”

 

Mifano ya watu wenye majina haya ni Salama Jabir (mtangazaji), Salma Kikwete (Mbunge), Salim Ahmed Salim (Waziri Mkuu Mstaafu), Selima/Selma Mwazaya (mtangazaji) na Solma Kassim (Mtangazaji).

 

Wakati huo huo, hapa Ofisi ya Rais, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka, tuna SALAMA SAIDI MOHAMED.

 

Hili jina lina siri mbili ambazo watu wengi hawafahamu.

 

“Wanamuziki wengi wanaliimba jina hili na wazazi wengi wanawapa watoto wao jina hili. Je, jina hili lina nini zaidi ya ile AMANI?”

 

Mwanakwetu kwa muda mrefu alifanya jitihada kuwatafuta wanamuziki kadhaa ili kutoa majibu juu ya inakuwaje nyimbo nyingi zinaimbwa na kupewa jina SALIMA. Kwa bahati mbaya, majibu hayakupatikana hadi sasa.

 

Sasa Mwanakwetu ana matumaini ya kupata nusu ya jibu la swali hili: Je, kwa nini wazazi wengi wanawapa watoto wao jina hili?

Mtoa jibu hili si mwingine bali ni Salama Saidi Mohamed, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu. Nitamtafuta chemba, kisha akinipa majibu nitakusimulia, msomaji wangu.

 

Huku nikiendelea kuwatafuta wanamuziki wote hao waliowahi kuimba juu ya jina hili, na wao nitawasihi kwa hisani yao wanipe jibu.

 

Swali ni: Je, huyu Salama Saidi Mohamed wa Ofisi ya Rais, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka, wadau waliniambia kuwa hivi karibuni alifiwa na mzazi wake mmoja; je, swali hili atakuwa na jibu, au aliwahi kumuuliza mzazi wake akiwa hai?

Mimi nisiandikie mate wakati wino upo. Sasa niko njiani kumfuata kiongozi huyu ili anipe majibu na Mwanakwetu siyo mchoyo nitawasimulia majibu yake.

Mwanakwetu upo? Kumbuka.

Natafuta Siri ya Jina SALAMA

Nakutakia Siku Njema.


makwadeladius@gmail.com
0717649257




 

 

 

0/Post a Comment/Comments