KILA MTU ANAWEZA KULETA MABADILIKO CHANYA KATIKA JAMII


Emakulata Msafiri 

Mwanakwetukids

Kulikuwa na ardhi nzuri lakini wakazi wake hawakujali usafi wa mazingira. Takataka zilitupwa ovyo, mifereji ilikuwa imeziba na maji machafu yalikuwa yakituama karibu na nyumba. Kutokana na hali hiyo magonjwa kama malaria na kuhara yalikuwa ya kawaida.

Katika kijiji hicho aliishi kijana aitwaye Baraka. Alikuwa mwanafunzi mwenye bidii na aliyependa kujifunza mambo mapya. Siku moja mwalimu wake aliwafundisha wanafunzi kuhusu umuhimu wa usafi wa mazingira katika kuzuia magonjwa. Baraka alivutiwa sana na somo hilo na akaamua kuwaelimisha watu wa kijiji chake.

Mwanzoni baadhi ya wakazi walimcheka na kusema kuwa mtoto hawezi kuwafundisha watu wazima. Hata hivyo Baraka hakukata tamaa. Alianza kwa kufanya usafi katika eneo la nyumba yao pamoja na familia yake. Baada ya muda majirani waliona mazingira yao yamekuwa safi na hakuna aliyekuwa akiugua mara kwa mara kama ilivyokuwa awali.


Baraka aliwashirikisha viongozi wa kijiji na walimu wa shule kuandaa siku maalumu ya usafi. Wananchi walikusanyika na kusafisha barabara, mifereji ya maji na maeneo ya soko. Pia walipanda miti na kuweka mapipa ya kutupia taka katika sehemu mbalimbali.

Baada ya miezi kadhaa kijiji kilibadilika sana. Magonjwa yalipungua, mazingira yakawa safi na ya kuvutia na wageni wengi walianza kutembelea kijiji hicho kujifunza jinsi walivyofanikiwa kudumisha usafi. Serikali ya eneo hilo ilikitambua kijiji cha Amani kama mfano wa kuigwa katika utunzaji wa mazingira.


Baraka alipewa tuzo ya uongozi bora kwa mchango wake katika maendeleo ya kijiji. Alifurahi kuona kuwa mabadiliko makubwa yanaweza kuanza na mtu mmoja mwenye nia njema na mwenye uthubutu wa kuchukua hatua.


emakulatemsafiri@gmail.com

 

0653903872

0/Post a Comment/Comments