Emakulata Msafiri
Mwanakwetukids
Wazazi na walezi wengi huamini kuwa kumlinganisha mtoto na watoto wengine kunaweza kumtia bidii na kumfanya afanye vizuri zaidi. Hata hivyo kwa kiasi kikubwa tabia hii haina manufaa. Badala ya kumjenga mara nyingi humuumiza kihisia na kumfanya apoteze kujiamini.
Mtoto anapolinganishwa na wenzake anaweza kuhisi kuwa hafai au hapendwi jinsi alivyo. Kauli kama "Angalia mwenzako anavyofanya vizuri kuliko wewe" zinaweza kumfanya ajione hana uwezo. Hali hii inaweza kusababisha kushuka kwa ari ya kujifunza, kujitenga na wengine au hata kupata msongo wa mawazo.
Aidha kumlinganisha mtoto kunaweza kuibua wivu, hasira na ushindani usio na afya. Kila mtoto ana uwezo, vipaji na kasi yake ya kujifunza. Hivyo kumlazimisha afanane na mtoto mwingine si jambo la haki wala lenye kumsaidia.
Badala ya kulinganisha wazazi na walezi wanapaswa kumtia moyo mtoto kwa kutambua maendeleo yake binafsi. Kumsifu anapojitahidi hata kama hatua ni ndogo humjengea kujiamini na kumhamasisha kuendelea kujifunza na kuboresha uwezo wake.
Kwa kumalizia kumlinganisha mtoto na wengine hakumjengi bali kunaweza kumuumiza na kumrudisha nyuma. Njia bora ni kumwelekeza, kumtia moyo na kumthamini kwa uwezo wake wa kipekee. Mtoto anayelelewa kwa upendo, heshima na kutiwa moyo huwa na nafasi kubwa ya kukua akiwa na kujiamini na kufikia malengo yake.
emakulatemsafiri@gmail.com
0653903872



Post a Comment