.gif)
Adeladius Makwega
Ofisi ya Rais – Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Dodoma
DODOMA, Agosti 24, 2026 — Uhifadhi wa kumbukumbu na nyaraka ni msingi muhimu wa utendaji wa taasisi, historia ya taifa na uendelezaji wa maarifa kwa vizazi vijavyo. Pamoja na maendeleo yanayoendelea katika eneo hili, bado kuna umuhimu mkubwa wa viongozi na menejimenti za taasisi kuendelea kuipa sekta hii kipaumbele kinachostahili.
Kwa mujibu wa Emilian B. Muungano, Mkuu wa Sehemu ya Huduma za Nyaraka katika Ofisi ya Rais – Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, hali ya uhifadhi wa kumbukumbu na nyaraka nchini kwa sasa ni nzuri, lakini mafanikio zaidi yanahitaji msisitizo na dhamira ya pamoja.
Ndugu Muungano anasema miongoni mwa viongozi wanaoweza kutajwa kama mifano ya kuthamini kazi ya kumbukumbu na nyaraka ni Katibu Mkuu Eliakimu Chacha Maswi.
“Kwa muda mrefu amekuwa kiongozi wa mfano wa kuigwa katika taasisi alizowahi kufanya kazi. Maeneo yote aliyofanya kazi kuna simulizi moja inayokuwa kama nyayo yake.”
Anasema Muungano.
Anasimulia kuwa Maswi ana utamaduni wa kipekee wa kuanza siku yake ya kazi kwa kufika katika ofisi ya Kumbukumbu na Nyaraka, kuwajulia hali watumishi na kufahamu kinachoendelea kabla ya kuelekea ofisini kwake.
“Hii ni alama ya Eliakimu Maswi.”
Anasisitiza Muungano.
Muungano, ambaye amekuwa akifanya kazi katika eneo la kumbukumbu na nyaraka kwa zaidi ya miaka 23, tangu Desemba 2002, anatoa wito kwa wataalamu wa kada hiyo pamoja na menejimenti za taasisi nchini kuipa kazi ya kumbukumbu na nyaraka hadhi inayostahili.
“Wale waliosomea kazi hii wajitume. Menejimenti za kila taasisi nazo zisiifumbatie mikono; zina jukumu la kuipa kazi hii hadhi stahiki kama zinavyovipa vipaumbele vitengo vingine. Watumishi wa masjala wasiwe watu wa mwisho.”
Anasema.
Kauli hiyo inaweka wazi kwamba kumbukumbu na nyaraka si kazi ya pembeni, bali ni sehemu muhimu ya uendeshaji wa taasisi, uwajibikaji na utunzaji wa historia ya taifa.
Eliakimu Chacha Maswi ni mzaliwa wa Tarime, Mkoa wa Mara, ambaye amewahi kushika nafasi mbalimbali za uongozi serikalini, zikiwemo za Mtendaji Mkuu, Katibu Tawala wa Mikoa na Katibu Mkuu.
Katika safari yake ya utumishi wa umma, amewahi kuhudumu katika nyadhifa mbalimbali, ikiwemo Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Kudhibiti Ununuzi wa Umma (PPRA), Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, na baadaye kuhamishiwa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum.
Kwa simulizi hii, Maswi anaonekana pia kuwa mdau muhimu wa kumbukumbu na nyaraka—si kwa maneno pekee, bali kupitia utamaduni wa kuwatambua na kuwaheshimu watendaji wanaobeba hazina ya kumbukumbu za taasisi.
Kumbukumbu hujenga historia, nyaraka hulinda ushahidi, na viongozi wanaozithamini huacha nyayo zinazodumu.
📞 0717 649 257
.gif)
.gif)
.gif)













Post a Comment