Emakulata Msafiri
Mwanakwetukids
Katuni ni mojawapo ya burudani zinazopendwa sana na watoto. Huwafanya watoto wafurahie muda wao huku wakijifunza mambo mbalimbali yenye manufaa. Katuni nyingi hufundisha maadili mema kama vile kuheshimu wazazi, kushirikiana na wenzake, kusema ukweli na kupenda kusoma.
Siku hizi watoto wana nafasi ya kutazama katuni kupitia televisheni na mitandao ya intaneti. Baadhi ya katuni maarufu huonesha wahusika wanaowasaidia watoto kujifunza kwa njia ya nyimbo, michezo na hadithi za kusisimua. Pia vituo vya televisheni vinaendelea kuandaa vipindi vya katuni kwa ajili ya watoto hasa kipindi hiki cha likizo.
Hata hivyo wazazi na walezi wanapaswa kuhakikisha watoto wanatazama katuni zinazofaa umri wao. Katuni zenye lugha nzuri na maadili mema huwasaidia watoto kukua katika mazingira bora. Aidha muda wa kutazama katuni unapaswa kupangwa ili watoto wapate nafasi ya kusoma, kucheza na kupumzika.
Kwa ujumla katuni ni burudani muhimu kwa watoto ikiwa zitatumiwa kwa usahihi. Huburudisha, hufundisha na kuwajengea watoto ubunifu pamoja na maadili mema yatakayowasaidia katika maisha yao ya kila siku.
emakulatemsafiri@gmail.com
0653903872



Post a Comment