Emakulata Msafiri
Mwanakwetukids
Kila jioni baada ya kutoka shuleni watoto wa mtaa walipenda kwenda kucheza kwenye bustani ndogo iliyokuwa karibu na nyumba zao. Bustani hiyo ilikuwa imejaa maua ya rangi mbalimbali na vipepeo waliokuwa wakiruka kwa furaha.
Siku moja watoto walikuta watu wakikata maua ovyo na kutupa taka kila mahali. Polepole vipepeo wakaanza kutoweka. Watoto walihuzunika walipoona bustani ikipoteza uzuri wake.
Walikaa pamoja na kuamua kufanya jambo. Kila mmoja alikusanya taka wakapanda miche mipya ya maua na kuweka kibao kilichoandikwa "Linda Bustani Yetu".
Baada ya wiki chache maua yalichanua tena. Asubuhi moja kipepeo wa rangi ya buluu aliruka juu ya maua mapya. Watoto walishangilia walipoona vipepeo wengi wakirudi.
Tangu siku hiyo kila mtoto alijifunza kuwa mazingira mazuri huanza kwa matendo madogo ya kila siku. Bustani yao ikawa sehemu ya furaha kwa watoto na viumbe wengine.
emakulatemsafiri@gmail.com
0653903872



Post a Comment