Emakulata Msafiri
Mwanakwetukids
Mtoto mdogo anaweza kuwa na msongo wa mawazo. Ingawa watoto mara nyingi hushindwa kueleza hisia zao kwa maneno kama watu wazima. Wanaweza kuonesha msongo kupitia mabadiliko ya tabia na hisia. Kwa mfano mtoto anaweza kuwa mkimya kupita kiasi, kulia mara kwa mara, kukosa usingizi, kupoteza hamu ya kula, kujitenga na wenzake au kushindwa kuzingatia masomo. Kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO) msongo wa mawazo ni hali ya mvutano wa kiakili na kimwili inayotokana na changamoto au mazingira magumubna unaweza kuwapata watu wa rika zote wakiwemo watoto (World Health Organization [WHO], 2023).
Sababu zinazoweza kusababisha msongo wa mawazo kwa watoto ni nyingi. Miongoni mwa sababu hizo ni migogoro ya kifamilia, uonevu shuleni, kupoteza mzazi au mlezi na unyanyasaji shinikizo la masomo, pamoja na mabadiliko makubwa ya mazingira kama kuhama nyumba au shule. Mtoto anayekabiliwa na hali hizi anaweza kuathirika kihisia na kushindwa kufanya shughuli zake za kila siku kama kawaida. Ikiwa dalili hizi zitaendelea kwa muda mrefu au kuongezeka ni muhimu wazazi au walezi wampe mtoto msaada wa kihisia na kumpeleka kwa mtaalamu wa afya ya akili kwa ushauri na tathmini ya mapema.
Kwa hiyo ni muhimu jamii kutambua kuwa afya ya akili ya watoto ni muhimu kama afya yao ya mwili. Kuwasikiliza watoto, kuwapa mazingira salama na yenye upendo, pamoja na kutafuta msaada wa kitaalamu pale inapohitajika kunaweza kuwasaidia kukua wakiwa na afya njema ya akili na hisia.
emakulatemsafiri@gmail.com
0653903872




Post a Comment