Emakulata Msafiri
Mwanakwetukids
Katika bustani moja kubwa iliyokuwa karibu na mji waliishi ndege wengi wa aina tofauti. Miongoni mwao kulikuwa na ndege mmoja aliyependa kusaidia wengine wakati wa shida.
Mwaka mmoja kulitokea ukame mkubwa. Miti mingi ilikauka na chakula kikawa haba. Ndege wengi walihangaika kutafuta mbegu na matunda. Wengine walikuwa wakigombania chakula kidogo kilichobaki.
Siku moja ndege huyo alipata sehemu yenye mbegu nyingi. Alijua kwamba angeweza kula peke yake na kushiba lakini moyo wake haukumruhusu kufanya hivyo. Aliwaita ndege wengine waliokuwa na njaa na kuwashirikisha chakula hicho.
Ndege wengine walifurahia ukarimu wake na kumshukuru sana. Tangu siku hiyo walimheshimu kwa tabia yake nzuri.
Baada ya miezi kadhaa ndege huyo alipata jeraha kwenye bawa lake na kushindwa kuruka kwa muda. Hakuweza tena kutafuta chakula wala maji. Alibaki kwenye kiota chake akihitaji msaada.
Waliposikia hali yake ndege aliowahi kuwasaidia walifika kwa wingi. Kila siku walimletea chakula na maji mpaka alipopona kabisa. Alifurahi kuona kuwa wema wake ulikuwa umezaa matunda.
Baada ya kupona aliwashukuru wote waliomsaidia na kuwakumbusha kuwa upendo na huruma ni msingi wa maisha bora katika jamii.
emakulatemsafiri@gmail.com
0653903872



Post a Comment