VYOMBO VYA HABARI VYATAKIWA KULINDA MASLAHI YA WATOTO

 

Na Mwandishi Wetu

Mwanakwetukids.

Vyombo vya habari nchini vimetakiwa kuzingatia maadili ya taaluma ya uandishi wa habari wakati wa kuripoti masuala yanayowahusu watoto ili kulinda haki, usalama na ustawi wao. Wito huo umetolewa na mwakilishi wa UNICEF Tanzania wakati wa mafunzo yaliyowakutanisha wanahabari na wadau wa maendeleo ya watoto jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika mafunzo hayo mwakilishi huyo alisema kuwa watoto ni kundi maalumu linalohitaji ulinzi wa hali ya juu hivyo taarifa zinazowahusu zinapaswa kutolewa kwa umakini mkubwa. Alieleza kuwa kuchapisha picha, video au taarifa binafsi za watoto bila kufuata taratibu kunaweza kusababisha madhara ya kisaikolojia, unyanyapaa na ukiukwaji wa haki zao.

Aliongeza kuwa vyombo vya habari vina nafasi kubwa katika kuelimisha jamii kuhusu haki za watoto na kupambana na vitendo vya ukatili, unyanyasaji na ubaguzi dhidi yao. Hivyo wanahabari wanapaswa kuhakikisha habari wanazozitoa zinazingatia maslahi ya mtoto na kulinda hadhi yake.

Washiriki wa mafunzo hayo walieleza kuwa elimu waliyoipata itawasaidia kutekeleza majukumu yao kwa weledi zaidi. Waliahidi kuendelea kufuata maadili ya taaluma ili kuhakikisha watoto wanalindwa kupitia taarifa zinazotolewa kwa umma.



emakulatemsafiri@gmail.com 

0653903872



0/Post a Comment/Comments