TEMBO NA MCHWA

Emakulata Msafiri

Mwanakwetu Kids 

Hapo zamani za kale kulikuwa na msitu mkubwa wenye wanyama wa aina mbalimbali. Katika msitu huo aliishi tembo mkubwa sana aitwaye Tembo Jitu. Alikuwa na mwili mkubwa, nguvu nyingi na sauti iliyotikisa msitu mzima.

Kwa sababu ya ukubwa wake Tembo Jitu aliwadharau wanyama wengine. Alipokutana na swala alimwambia "Wewe ni mdogo sana huwezi kufanya chochote mbele yangu".

Alipokutana na sungura alisema "Miguu yako ni mifupi sana. Huwezi kushindana nami."

Hata ndege waliporuka juu yake aliwacheka na kusema "Ninyi ni wadogo mno kiasi kwamba siwaoni kuwa wa maana."

Wanyama wote walihuzunika kwa tabia yake walitamani ajifunze kuwa heshima.

Siku moja mchwa mdogo aitwaye Chungu alimsikia tembo akiwakejeli wanyama. Chungu alikasirika lakini hakutaka kugombana. Alitaka kumfundisha tembo somo.

Asubuhi iliyofuata tembo alikuwa akitembea kuelekea mtoni kunywa maji. Alikuwa akiimba kwa sauti kubwa na kujisifu.

 Ghafla Chungu alipanda kwenye mguu wake akatembea polepole hadi kwenye kichwa chake kisha akaingia ndani ya pua yake.

Tembo alianza kuhisi muwasho mkali. "Aaah! Ni nini hiki?" alipiga kelele.

Alijaribu kupepesa masikio yake lakini haikusaidia. Alitikisa kichwa chake lakini mchwa aliendelea kumsumbua. Tembo alianza kukimbia huku na huku msituni. Aligonga miti akaruka kwenye madimbwi ya maji na hata akajiviringisha chini. Lakini mchwa hakuondoka.

Wanyama walimwangalia kwa mshangao. Baada ya muda tembo alichoka sana. Alisimama na kuanza kuomba msaada. "Tafadhali yeyote anayenisaidia nitashukuru sana!"

Mchwa akatoka kwenye pua yake na kusema "sasa unaona kuwa hata mdogo anaweza kuwa na nguvu zake?" Tembo alitulia kwa aibu. Aligundua kuwa alikuwa amekosea kuwadharau wengine.

Samahani sana alisema. "Nimejifunza kuwa ukubwa si kila kitu kila kiumbe kina thamani yake."

Kuanzia siku hiyo tembo aliwaheshimu wanyama wote wakubwa kwa wadogo. Wanyama walifurahi na kuishi kwa amani.

emakulatemsafiri@gmail.com

0653903872


0/Post a Comment/Comments