SIMBA NA PANYA MSAIDIZI

 

Emakulata Msafiri

Mwanakwetukids

Siku moja katika msitu mkubwa wenye miti mirefu na nyasi nyingi aliishi simba mkubwa aliyeitwa Mfalme Simba. Wanyama wote wa msituni walimwogopa kwa sababu alikuwa na nguvu nyingi sana. Alipopita wanyama wengine walijificha au kusimama kwa heshima.

Asubuhi moja baada ya kuwinda chakula simba alihisi uchovu mkubwa. Alikwenda chini ya mti mkubwa wa mkuyu na kulala usingizi mzito. Upepo mwanana ulivuma na kufanya mazingira yawe tulivu.

Wakati simba amelala panya mdogo aliyeitwa Pendo alikuwa akicheza na marafiki zake karibu na mti huo. Walikuwa wakikimbizana huku wakicheka kwa furaha. Kwa bahati mbaya Pendo alipokimbia kwa kasi alipanda juu ya mgongo wa simba bila kujua.

Simba alishtuka usingizini na kwa hasira akamkamata panya kwa makucha yake makubwa.

"Wewe panya mdogo! Umethubutuje kuniamsha usingizini?" simba alinguruma kwa sauti kubwa.

Pendo alianza kutetemeka kwa hofu.

"Tafadhali Mfalme Simba nisamehe. Sikukusudia kukuudhi. Niachie niende na siku moja nitakusaidia." Simba alianza kucheka kwa sauti kubwa.

"Wewe utanisaidia mimi? Hahaha! Mimi ni simba mkubwa na mwenye nguvu kuliko wote msituni. Unawezaje kunisaidia?"

Lakini baada ya kufikiria kidogo simba aliamua kumwachia.

"Nenda zako leo sitakudhuru."

Pendo alimshukuru sana na kukimbia haraka kwenda nyumbani.

Siku zilipita. Asubuhi moja simba alikuwa akitembea msituni akitafuta chakula. Hakujua kuwa wawindaji walikuwa wameweka wavu mkubwa kati ya miti.

Ghafla simba aliingia ndani ya wavu ule na kunaswa. Alijaribu kujitoa kwa nguvu zake zote lakini kadiri alivyojiburuza ndivyo alivyokwama zaidi.

Aliunguruma kwa nguvu akiomba msaada. Wanyama wengi walisikia sauti yake lakini waliogopa kusogea karibu. Pendo panya naye alisikia mlio huo akiwa mbali. Alipotambua kuwa ni simba aliyekuwa amemwokoa zamani alikimbia haraka kuelekea alikokuwa.

Alipofika alimkuta simba akiwa amenaswa kabisa.

"Usijali Mfalme Simba". alisema Pendo nitakusaidia."

Simba alishangaa. "Lakini wewe ni mdogo sana!"

Pendo hakujibu. Alianza kutafuna kamba za wavu kwa meno yake madogo lakini makali. Alifanya kazi kwa bidii bila kuchoka.

Baada ya muda kamba moja ilikatika. Kisha nyingine. Hatimaye wavu wote ulilegea na simba akaweza kutoka. Simba alikuwa na furaha sana.

"Asante sana Pendo. Leo nimejifunza kuwa hata mdogo anaweza kufanya jambo kubwa".

Tangu siku hiyo simba na panya wakawa marafiki wakubwa. Simba hakuwahi tena kuwadharau wanyama wadogo na wanyama wote wa msituni walijifunza umuhimu wa kusaidiana.

emakulatemsafiri@gmail.com

0653903872


0/Post a Comment/Comments