Emakulata Msafiri
Mwanakwetukids.com
Kumfundisha mtoto kumjua Mungu ni jukumu muhimu kwa wazazi, walezi na jamii kwa ujumla. Elimu ya kumjua Mungu inamsaidia mtoto kukua akiwa na maadili mema, heshima, upendo na utii. Mtoto anapomjua Mungu tangu akiwa mdogo huwa na msingi mzuri wa maisha yake ya baadaye na anaweza kufanya maamuzi yanayompendeza Mungu na jamii.
Njia mojawapo ya kumfundisha mtoto kumjua Mungu ni kwa kumweleza kuhusu uwepo na upendo wa Mungu kwa lugha rahisi anayoielewa. Wazazi wanapaswa kutumia muda kusoma na kusimulia hadithi za katika Biblia ambazo zinaonesha matendo makuu ya Mungu na jinsi alivyowasaidia watu wake. Hadithi hizi humsaidia mtoto kuelewa kwamba Mungu ni mwenye upendo, rehema, na ulinzi kwa watu wote.
Pia wazazi wanapaswa kuwa mfano mzuri kwa watoto wao. Mtoto hujifunza zaidi kwa kuona matendo ya wazazi wake kuliko kwa kusikia maneno yao pekee. Anapowaona wazazi wakisali, wakisoma Biblia, wakisema ukweli na kuwasaidia wengine naye hujifunza kufanya hivyo. Hivyo maisha ya wazazi yana mchango mkubwa katika kumjenga mtoto kiroho.
Vilevile mtoto anapaswa kufundishwa kusali na kumshukuru Mungu kwa mambo mbalimbali anayopata kila siku. Sala humsaidia mtoto kujenga uhusiano wa karibu na Mungu na kumtegemea katika maisha yake.
Kwa ujumla kumfundisha mtoto kumjua Mungu ni msingi muhimu wa kumlea katika maadili mema na maisha yenye hofu ya Mungu. Wazazi na walezi wanapaswa kutambua wajibu wao wa kumwelekeza mtoto katika njia ya Mungu tangu akiwa mdogo ili akue akiwa mtu mwema mwenye heshima na mwenye manufaa kwa jamii. Kupitia mafundisho hayo mtoto anaweza kuwa na maisha yenye mwelekeo mzuri na matumaini ya baadaye.
emakulatemsafiri@gmail.com
0653903872


Post a Comment