Emakulata Msafiri
Mwanakwetukids
Kulikuwa na ndege wawili marafiki walioitwa Titi na Tatu. Kila siku walikuwa wakiruka pamoja kutafuta chakula katika mashamba na misitu ya karibu.
Siku moja kulikuwa na ukame. Mvua haikunyesha kwa muda mrefu na chakula kilikuwa kigumu kupatikana. Ndege hao walizunguka kutoka sehemu moja hadi nyingine wakitafuta chochote cha kula.
Baada ya kutafuta kwa muda mrefu Titi aliona punje moja kubwa ya mahindi chini ya mti.
"Tazama! Tumepata chakula!" alipiga kelele kwa furaha.
Wote wawili walishuka haraka. Lakini walipofika karibu na punje hiyo tatizo likaanza.
"Mimi ndiye nimeiona kwanza hivyo ni yangu" alisema Titi.
"Hapana tulikuwa tunatafuta pamoja. Tunapaswa kula wote" alisema Tatu.
"Mimi siwezi kugawana. Nina njaa sana."
"Nami pia nina njaa."
Walianza kubishana. Kadiri walivyoendelea kubishana ndivyo walivyozidi kukasirika. Mwishowe walianza kuvutana na kusukumiana karibu na punje ya mahindi. Wakati huo kuku mmoja aliyekuwa akipita karibu aliona kinachoendelea.
Kuku huyo alisimama kimya na kuwasikiliza kwa muda.
Alipoona ndege hao wamezama kwenye ugomvi alitembea taratibu kuelekea punje ya mahindi. Titi na Tatu hawakugundua.
Ghafla kuku aliidaka punje ile kwa mdomo wake na kuimeza yote mara moja.
Alafu akaondoka zake.Ndege hao waliposhtuka walikuta punje imekwisha.
Wapi mahindi? aliuliza Titi kwa mshangao "Kuku ameyaondoa!" alisema Tatu.
Wote walinyamaza kwa huzuni. Baada ya muda Titi alisema kwa sauti ya polepole "Tungegawana tangu mwanzo." Tatu alikubali ni kweli tumepoteza chakula kwa sababu ya ugomvi. Kuanzia siku hiyo waliahidiana kutoshindania vitu vidogo. Walijifunza kushirikiana na kugawana kila walichopata.
Baada ya siku chache walipata punje nyingi zaidi za mahindi. Safari hii waligawana kwa usawa na kula kwa furaha. Marafiki hao waliendelea kuishi kwa amani na kusaidiana kila walipohitaji.
emakulatemsafiri@gmail.com
0653903872



Post a Comment