Emakulata Msafiri
Mwanakwetukids.com
Katika jiji moja kubwa lenye majengo marefu na barabara zenye shughuli nyingi aliishi mtoto mmoja mwenye tabia njema. Kila siku alisikiliza maelekezo ya wazazi wake na kuyafuata kwa uangalifu. Siku moja mama yake alimwambia.
"Baada ya kutoka shuleni rudi nyumbani moja kwa moja usichelewe njiani wala kufuata watu usiowajua". Mtoto huyo akakubali na kwenda shuleni.
Masomo yalipoisha baadhi ya wanafunzi walimwita waende kutembea kwenye kituo kipya cha michezo kilichokuwa mbali na nyumbani. Wengine walitaka kwenda sokoni kutazama bidhaa mbalimbali. Ingawa alitamani kujiunga nao alikumbuka maelekezo ya mama yake. Akaamua kurudi nyumbani kama alivyoagizwa.
Njiani alifika kwenye makutano ya barabara yenye magari mengi. Alisimama kwa makini akaangalia kushoto na kulia kisha akavuka kupitia kivuko cha waenda kwa miguu.
Alipofika nyumbani salama mama yake alifurahi sana kuona kwamba alikuwa ametii maelekezo. Jioni hiyo walipokuwa wakitazama habari walisikia kuwa kulikuwa na vurugu ndogo katika eneo ambalo baadhi ya watoto walikuwa wameenda kutembea.
Mama yake akamwambia "Usikivu si kusikia tu. Ni kuelewa na kutii maelekezo yanayolinda maisha yetu." Mtoto huyo alitabasamu akitambua kwamba uamuzi wake wa kusikiliza ulikuwa wa busara.Kuanzia siku hiyo akawa mfano mzuri kwa watoto wengine katika mtaa wao.
emakulatemsafiri@gmail.com
0653903872

Post a Comment