Emakulata Msafiri
Mwanakwetukids.com
Kulikuwa na kunguru mmoja aliyeishi karibu na kijiji. Mwaka huo kulikuwa na jua kali sana. Mito mingi ilikauka na mabwawa mengi yakapungua maji.
Siku moja kunguru aliamka asubuhi akiwa na kiu kali. Alianza kuruka huku na huku akitafuta maji.
Alifika kwenye mto mdogo, lakini ulikuwa umekauka. Akaenda kwenye bwawa, nalo lilikuwa na matope tu. Kadiri muda ulivyopita, kiu yake ilizidi kuongezeka.
"Ni lazima nipate maji leo," alijisemea.
Aliendelea kutafuta kwa muda mrefu mpaka akafika karibu na shamba la mkulima. Hapo aliona mtungi mkubwa wa udongo uliowekwa chini ya mti.
Kwa furaha kubwa akaruka na kutua juu ya mtungi.
Alipochungulia ndani, aliona maji. Lakini maji yalikuwa chini sana. Alijaribu kuingiza mdomo wake ndani ya mtungi, lakini haukuyafikia.
Kunguru alijaribu kuusukuma mtungi uanguke ili maji yamwagike. Lakini mtungi ulikuwa mzito sana.Akajaribu tena na tena bila mafanikio.
Kwa muda alikata tamaa. Lakini hakutaka kuondoka bila maji.
Aliketi karibu na mtungi na kuanza kufikiri.
Mara akagundua kulikuwa na kokoto nyingi pembeni ya mtungi. Wazo likamjia.
Alichukua kokoto moja kwa mdomo wake na kuitupa ndani ya mtungi.
Kisha akachukua nyingine.
Aliendelea kutupa kokoto moja baada ya nyingine. Baada ya muda aliona maji yakianza kupanda juu kidogo. Kunguru alifurahi. Alijua mpango wake ulikuwa unafanya kazi.
Bila kuchoka aliendelea kuleta kokoto zaidi. Jua lilikuwa kali na kazi ilikuwa ngumu lakini hakukata tamaa. Hatimaye baada ya kokoto nyingi kutupwa ndani ya mtungi maji yalipanda mpaka karibu na mdomo wa mtungi.
Kunguru akainama na kunywa maji matamu mpaka kiu yake ikaisha. Alipomaliza alitazama mtungi na kutabasamu.
"Kama ningekata tamaa ningebaki na kiu. Kufikiri vizuri na kuwa mvumilivu kumeokoa maisha yangu."Kisha akaruka kwa furaha na kurudi nyumbani kwake.
emakulatemsafiri@gmail.com
0653903872

Post a Comment