ALIDHANI ANA MUDA MWINGI LAKINI MAMBO YAKABADILIKA

 

Emakulata Msafiri 

Mwanakwetukids

Kulikuwa na kijana mmoja aliyekuwa akisoma katika shule ya sekondari. Alikuwa na uwezo mzuri darasani lakini alikuwa na tabia ya uvivu. Hakupenda kufanya kazi za nyumbani wala kujisomea. Muda wake mwingi aliutumia kuangalia video kwenye simu, kucheza michezo ya mtandaoni na kuzungumza na marafiki katika mitandao ya kijamii.

Wazazi wake walimshauri mara kwa mara kubadili tabia yake na kutumia muda vizuri lakini hakuwasikiliza. Kila alipokumbushwa kuhusu masomo au kazi za nyumbani aliahidi kufanya baadaye.

Siku moja shule ilitangaza mtihani mkubwa wa muhula. Wanafunzi wengi walianza kujiandaa mapema kwa kusoma na kufanya mazoezi ya maswali mbalimbali. Yeye aliendelea kucheza na kutumia simu akiamini kuwa angeweza kusoma siku za mwisho.

Hatimaye siku ya mtihani ilifika. Alipopewa karatasi ya maswali aligundua kuwa hakuwa tayari. Maswali mengi yalikuwa magumu kwake kwa sababu hakusoma kwa bidii. Alimaliza mtihani akiwa na wasiwasi mkubwa.

Matokeo yalipotoka hakufanya vizuri. Alisikitika sana na kutambua kuwa sababu ya matokeo hayo ilikuwa uvivu wake. Tangu siku hiyo aliamua kubadilika. Alipanga ratiba ya masomo akapunguza matumizi ya simu na kuanza kufanya kazi zake kwa wakati.

Baada ya muda aliona mabadiliko makubwa katika masomo yake. Alianza kupata alama nzuri na kuamini kuwa mafanikio yanapatikana kwa juhudi na nidhamu.



emakulatemsafiri@gmail.com 

0653903872



0/Post a Comment/Comments