Emakulata Msafiri
Mwanakwetukids.com
Katika kijiji kimoja karibu na Iringa kulikuwa na familia iliyopenda sana kusikiliza redio jioni. Kila baada ya kazi za siku kuisha watoto na wazazi wao walikusanyika sebuleni kusikiliza habari nyimbo, na vipindi vya elimu.
Miongoni mwa watoto wa familia hiyo alikuwa mmoja aliyependa sana kusikiliza watangazaji wa redio. Alivutiwa na jinsi walivyoongea kwa ujasiri na kuwapa watu habari muhimu. Kila alipokuwa peke yake alikuwa akijifanya mtangazaji huku akitumia kijiti kama kipaza sauti.
Lakini baadhi ya watoto wenzake walimcheka. “Wewe huwezi kuwa mtangazaji. Hata sauti yako ni ya kawaida!” Maneno hayo yalimuumiza lakini hakuwahi kuacha ndoto yake.
Shuleni kulikuwa na klabu ya sanaa na mawasiliano. Siku moja mwalimu alitangaza kuwa shule ingeanza kipindi kidogo cha matangazo ya asubuhi ambapo wanafunzi wangekuwa wakitoa matangazo kabla ya masomo kuanza.
Watoto wengi waliogopa kuzungumza mbele ya wengine. Yeye alijitolea mara moja ingawa moyo wake ulikuwa ukidunda kwa nguvu.
Usiku kabla ya siku yake ya kwanza kutangaza alikaa muda mrefu akiandika maneno yake kwenye daftari. Aliisoma hotuba hiyo tena na tena mpaka akaikariri karibu yote.
Asubuhi ilipofika wanafunzi wote walikusanyika uwanjani. Aliposimama mbele ya kipaza sauti mikono yake ilikuwa inatetemeka. Kwa sekunde chache alihisi kama angekimbia.
Lakini alikumbuka maneno ya mama yake “Ukiogopa kujaribu hutajua uwezo wako.”
Akapumua kwa nguvu na kuanza kuzungumza.
Mwanzoni sauti yake ilikuwa ya chini lakini kadiri alivyoendelea alizoea. Wanafunzi walimsikiliza kwa makini na walimu walifurahishwa na ujasiri wake. Baada ya matangazo kuisha mwalimu mkuu alimuita na kusema.
“Una kipaji kizuri sana endelea kukikuza.”
Kuanzia siku hiyo alianza kuamini kuwa ndoto zake zinawezekana. Aliendelea kujifunza kuzungumza vizuri na kushiriki katika shughuli mbalimbali za shule.
Miaka ilipopita ndoto yake ilitimia. Alikuja kufanya kazi katika kituo cha redio akitumia sauti yake kuwapa watu elimu, habari na matumaini.
Na kila alipokuwa akizungumza hewani hakusahau siku ile ya kwanza alipokuwa amesimama mbele ya wanafunzi akiwa na hofu kubwa moyoni.
emakulatemsafiri@gmail.com
0653903872



Post a Comment