Emakulata Msafiri
Mwanakwetukids.com
Katika moja ya mitaa yenye pilikapilika mjini Dar es Salaam kulikuwa na gereji ndogo pembeni ya barabara ambapo mafundi walikuwa wakitengeneza pikipiki na magari kila siku. Kelele za nyundo, mashine na harufu ya mafuta zilijaa eneo lote kuanzia asubuhi mpaka jioni.
Karibu na gereji hiyo aliishi kijana mmoja pamoja na mama yake katika chumba kidogo cha kupanga. Mama yake alikuwa akifua nguo za watu ili wapate chakula na kulipa kodi ya nyumba.
Baada ya kumaliza shule ya sekondari kijana huyo alitamani kuendelea na masomo lakini hali ya nyumbani haikuruhusu. Ili asikae tu mtaani alianza kwenda gereji kusaidia mafundi kazi ndogondogo kama kuosha vifaa, kufagia na kupeleka vipuri.
Baadhi ya mafundi walimpenda kwa sababu alikuwa mtulivu na mchapakazi. Lakini wengine walimdharau. “Huwezi kuwa fundi mzuri kwa kuangalia tu” walimwambia mara kwa mara.
Hakujibu vibaya. Aliendelea kujifunza kwa kuangalia na kuuliza maswali.
Kila jioni baada ya kazi alikuwa anakaa pembeni akiangalia jinsi mafundi walivyofungua injini za pikipiki na kuzirekebisha. Polepole alianza kuelewa kazi hiyo.
Siku moja fundi mkuu hakuwepo gereji ndipo mteja mmoja alileta pikipiki iliyokuwa imezimika njiani. Mafundi wengine walikuwa bize sana. Kijana huyo aliomba kujaribu kuangalia tatizo.
Wengine walicheka. “Usiharibu pikipiki ya watu.”
Lakini alikagua kwa makini na kugundua waya mmoja ulikuwa umelegea. Akaurekebisha na kuwasha pikipiki. Mara moja ikaanza kufanya kazi.
Mteja alifurahi sana na mafundi wote walimshangaa.
Kuanzia siku hiyo alianza kupewa kazi ndogo ndogo za matengenezo. Kadiri muda ulivyopita ujuzi wake uliongezeka sana. Wateja wengi wakaanza kumuamini kwa sababu alikuwa mwaminifu na hakupenda kudanganya watu.
Miaka michache baadaye alipata nafasi ya kufungua gereji yake mwenyewe. Ingawa biashara yake ilikua hakuwahi kusahau maisha aliyotoka. Mara nyingi alikuwa akiwachukua vijana wa mtaani na kuwafundisha kazi ili wasipoteze muda kwenye makundi mabaya.
Na kila alipomuona mama yake akitabasamu dukani kwake alikumbuka siku zile alipoanza kwa kufagia gereji bila hata kujua maisha yake yangebadilika.
emakulatemsafiri@gmail.com
0653903872



Post a Comment