Emakulata Msafiri
Mwanakwetukids.com
Kulikuwa na mtoto mmoja aliyekuwa mkorofi sana kuliko watoto wote kijijini. Hakupenda kusikia ushauri wa wazazi wake wala walimu wake. Kila siku alikuwa anatafuta ugomvi na kufanya mambo ya kuwaudhi watu wengine.
Akiwa shuleni alikuwa anawanyang’anya watoto wenzake kalamu na madaftari. Wakati mwalimu akifundisha yeye alikuwa anapiga kelele na kuchekesha darasa. Mara nyingi wanafunzi walikosa kuelewa somo kwa sababu ya fujo zake.
Nyumbani nako alikuwa na tabia mbaya. Mama yake alipomtuma dukani alikuwa anachelewa kwa sababu ya kucheza njiani. Baba yake alipomwambia afagie uwanja alikuwa anakimbia kwenda kucheza mpira na marafiki zake. Wazazi wake walimwonya mara nyingi lakini hakubadilika.
Siku moja kijijini kulikuwa na sherehe kubwa. Watoto wote waliitwa kusaidia kupamba uwanja na kupanga viti. Lakini mtoto huyo alianza kufanya utani mbaya. Aliwasukuma watoto wengine akavunja baadhi ya viti na kumwaga maji yaliyokuwa yameandaliwa kwa wageni.
Watu wote walikasirika sana. Watoto wenzake wakaanza kumkwepa kwa sababu waliona anaharibu kila kitu. Hata alipowaita waje kucheza naye hakuna aliyekubali.
Baadaye alipokuwa anarudi nyumbani peke yake alianza kuhuzunika. Aligundua kuwa ukorofi wake ulikuwa umemfanya akose marafiki na watu hawakumwamini tena.
Alipofika nyumbani mama yake alimketisha chini na kumwambia “Mtoto mwenye tabia nzuri hupendwa na kila mtu lakini mkorofi hujikuta peke yake.”
Maneno yale yalimgusa sana. Siku iliyofuata alienda kuwaomba radhi watoto wenzake na watu aliowakosea. Akaanza kusaidia kazi za nyumbani, kusikiliza walimu na kucheza vizuri na wengine.
Polepole watu wakaanza kuona mabadiliko yake. Watoto wakamkubali tena na walimu wakaanza kumpongeza kwa nidhamu nzuri. Tangu siku hiyo aliacha ukorofi na kuwa mtoto mwema na mwenye heshima.
emakulatemsafiri@gmail.com
0653903872



Post a Comment