Emakulata Msafiri
Mwanakwetukids.com
Hapo zamani za kale kulikuwa na mtoto mmoja aliyekuwa muoga sana. Aliogopa giza, sauti za usiku, mbwa na hata kukaa peke yake ndani ya nyumba. Kila alipokuwa akisikia mlango ukigonga au paka akilia alikuwa anakimbia kwenda kujificha kwa mama yake.
Siku moja wazazi wake walimtuma dukani kununua chumvi jioni. Njia ya kwenda dukani ilikuwa inapita karibu na kichaka kikubwa. Alitembea polepole huku moyo ukidunda kwa nguvu. Ghafla alisikia sauti ya “shaaa!” kwenye kichaka. Aliogopa sana na kutaka kukimbia.
Lakini alikumbuka maneno ya baba yake aliyesema “Mtu jasiri si yule asiyeogopa bali ni yule anayeshinda hofu yake.”
Akavuta pumzi na kuamua kuangalia vizuri. Kumbe ilikuwa ni mbuzi aliyekuwa anakula majani pembeni ya njia. Mtoto huyo akaanza kucheka mwenyewe kwa sababu aliogopa kitu kisicho cha hatari.Alifika dukani salama na kurudi nyumbani akiwa na furaha. Tangu siku hiyo alianza kupunguza uoga wake taratibu.
emakulatemsafiri@gmail.com
0653903872



Post a Comment