NDEGE MWEREVU

 


Emakulata Msafiri

Mwanakwetukids.com

Kulikuwa na ndege mmoja mdogo aliyeishi karibu na msitu mkubwa. Kila siku alipenda kuruka juu angani akiimba kwa furaha. Lakini siku moja jua lilikuwa kali sana mpaka mito mingi ikakauka.

Ndege alianza kuhisi kiu sana. Aliruka kutoka mti mmoja kwenda mwingine akitafuta maji.

“Laiti ningepata hata tone moja la maji” alisema kwa sauti ya uchovu.

Alitafuta karibu na mto lakini hakukuwa na maji. Akaenda shambani nako hakupata kitu. Mabawa yake yakaanza kuchoka.

Baada ya muda mrefu ndege aliona chupa ya zamani chini ya mti mkubwa. Haraka akaruka kwenda kuiangalia. “Ah! Kuna maji ndani!” alisema kwa furaha.

Lakini alipoweka mdomo wake ndani ya chupa aligundua maji yalikuwa chini sana. Alijaribu kuisukuma chupa lakini ilikuwa nzito. Akajaribu tena kunywa lakini bado hakufikia maji.

Ndege aliketi juu ya jiwe na kufikiria kwa makini.

“Nikiondoka sasa nitaendelea kuwa na kiu. Lazima nitafute njia nyingine” alisema.

Ghafla akaona mawe madogo yaliyokuwa karibu na chupa. Akapata wazo zuri sana

Akaanza kuyaokota mawe moja baada ya jingine na kuyadondosha ndani ya chupa.

Kila jiwe lilifanya maji yapande juu kidogo. Ndege aliendelea kufanya kazi bila kuchoka.

Baada ya muda maji yakafika karibu na mdomo wa chupa. Ndege akafurahi sana.

“Mwishowe nimefanikiwa!” alisema kwa tabasamu

Akanywa maji safi mpaka kiu yake ikaisha. Baada ya hapo akaruka juu angani kwa furaha kubwa

Tangu siku hiyo ndege aliwafundisha wanyama wengine kuwa matatizo hayaishi kwa kukata tamaa bali kwa kutumia akili na subira.

emakulatemsafiri@gmail.com

0653903872


0/Post a Comment/Comments