MWANAFUNZI MKWELI

 

Emakulata Msafiri

Mwanakwetukids.com

Mwanafunzi mkweli ni yule anayependa kusema ukweli na kufanya mambo kwa uaminifu wakati wote. Ukweli ni msingi muhimu katika maisha ya mwanafunzi kwa sababu humsaidia kuwa na tabia njema, kuaminika na kufaulu katika masomo yake. Mwanafunzi mwenye ukweli hupendwa na walimu, wanafunzi wenzake pamoja na jamii kwa ujumla.

Mwanafunzi mkweli huepuka udanganyifu katika masomo. Wakati wa mitihani au mazoezi ya darasani hafanyi wizi wa mitihani wala kunakili kazi za wengine. Huamini kuwa juhudi zake mwenyewe ndizo zitakazomletea mafanikio ya kweli. Hali hii humsaidia kupata maarifa sahihi na kuwa mfano mzuri kwa wanafunzi wengine.

Pia mwanafunzi mkweli huwa na nidhamu nzuri. Anapokosea hukubali makosa yake badala ya kusema uongo. Tabia hii humfanya kuaminika mbele ya walimu na wazazi wake. Pia hujenga urafiki mzuri na wenzake kwa sababu watu wengi hupenda kuishi na mtu mwenye uaminifu.

Aidha ukweli humsaidia mwanafunzi kuwa na amani ya moyo. Mwanafunzi anayesema ukweli haishi kwa hofu wala wasiwasi wa kufichua uongo wake. Hivyo huwa huru kufanya shughuli zake za kila siku kwa utulivu na furaha.

Hata hivyo baadhi ya wanafunzi hujihusisha na uongo kwa sababu ya kuogopa adhabu au kutaka kupata sifa ambazo hawakuzistahili. Tabia hii ni mbaya kwa sababu huweza kuharibu maisha yao ya baadaye na kupoteza imani kutoka kwa jamii.

Mwanafunzi mkweli ni muhimu sana katika jamii. Ukweli humjenga mwanafunzi kuwa mtu mwema, mwenye nidhamu na mwenye mafanikio ya kudumu. Hivyo kila mwanafunzi anapaswa kujifunza kusema ukweli na kuishi kwa uaminifu kila wakati.

emakulatemsafiri@gmail.com

0653903872


0/Post a Comment/Comments