Emakulata Msafiri
Mwanakwetukids.com
Kulikuwa na mtoto mmoja aliyeishi na bibi yake katika kijiji kilichokuwa mbali kidogo na mji wa Iringa. Wazazi wake walikuwa wanafanya kazi mbali hivyo alikulia chini ya malezi ya bibi yake aliyekuwa mzee lakini mwenye upendo mkubwa.
Kila siku asubuhi kabla ya kwenda shule mtoto huyo alimsaidia bibi yake kufanya kazi za nyumbani. Kufagia uwanja, kuchota maji na wakati mwingine alienda kukusanya kuni kichakani. Baada ya hapo ndipo alianza safari ndefu ya kwenda shule kwa miguu.
Njiani kulikuwa na kilima kirefu ambacho watoto wengi walikichoka kukipanda. Wakati mwingine baadhi yao walirudi nyumbani bila kufika shule hasa siku za baridi au mvua. Lakini yeye aliendelea kwenda kila siku kwa sababu aliamini elimu ndiyo ingemsaidia kubadilisha maisha yake.
Siku moja alipofika shuleni mwalimu alitangaza kuwa kungekuwa na mashindano ya kuandika insha kuhusu maisha ya kijijini. Mshindi angepata zawadi ya vitabu na sare mpya ya shule.
Watoto wengi walifurahi lakini mtoto huyo alihisi wasiwasi. Hakuwahi kushinda mashindano yoyote hapo kabla. Usiku ule alimwambia bibi yake.
“Sidhani kama naweza kushinda wenzangu wanaandika vizuri kuliko mimi.”
Bibi yake alisema “Usiogope kujaribu wakati mwingine ushindi huanza pale mtu anapoamua kutokata tamaa.”
Maneno yale yalimpa moyo kwa siku kadhaa aliandika na kufuta mara nyingi akijaribu kuboresha insha yake. Aliandika kuhusu changamoto za watoto wa vijijini, safari ndefu za kwenda shule na matumaini ya maisha bora kupitia elimu.
Siku ya matokeo ilipofika watoto wote walikusanyika chini ya mti mkubwa wa shule. Mwalimu mkuu alianza kutaja washindi. Mtoto huyo alishtuka kusikia jina lake likitajwa kuwa mshindi wa kwanza.Watoto walimpigia makofi na macho yake yakajaa machozi ya furaha. Aliporudi nyumbani akiwa na vitabu na sare mpya bibi yake alimkumbatia kwa furaha kubwa.
Kuanzia siku hiyo mtoto huyo alianza kujiamini zaidi. Alijifunza kuwa mafanikio hayaji kwa bahati pekee bali kwa juhudi, uvumilivu na kuamini uwezo wako mwenyewe.
emakulatemsafiri@gmail.com
0653903872



Post a Comment