Emakulata Msafiri
Mwanakwetukids.com
Mvua ndogo ilikuwa ikinyesha mitaa ya Dar es Salaam wakati Jamal aliposhuka kwenye daladala akiwa amebeba begi lake la shule mgongoni. Barabara ilikuwa na foleni kubwa watu wakikimbizana kuwahi kazi na wauza chipsi wakipaza sauti pembeni ya stendi.
Jamal alikuwa na haraka kufika nyumbani kabla mama yake hajarudi kutoka kazini. Lakini alipofika karibu na jengo lao alikumbuka kitu muhimu alikuwa ameacha daftari lake la hesabu darasani. “Sasa nitafanyaje?” alijiuliza kwa sauti ya chini.
Kesho yake walikuwa na mtihani wa hesabu na mwalimu wao alikuwa mkali sana kuhusu maandalizi. Kwa dakika kadhaa Jamal alisimama pembeni ya duka la vinywaji akiwa hajui aamue nini. Kurudi shule ilimaanisha kupanda daladala tena na kutumia nauli aliyokuwa amepewa kwa matumizi ya kesho.
Akiwa bado anafikiria rafiki yake Asha alipita. “Mbona uko hapa kama mtu aliyepotea?” akauliza kwa utani. Jamal akamweleza kilichotokea. Asha akafikiria kidogo kisha akasema
“Mimi nilipiga picha notes zote za hesabu. Tunaweza kusoma pamoja.”
Uso wa Jamal ukabadilika mara moja. Wakaenda kwenye kibanda kidogo cha kahawa karibu na mtaa wao wakafungua simu ya Asha na kuanza kujisomea.
Usiku huo Jamal alielewa hesabu vizuri kuliko siku nyingine zote.
Kesho yake baada ya mtihani mwalimu aliingia darasani akiwa na karatasi mkononi.
“Wanafunzi wengi mmefanya vibaya” alisema. “Lakini kuna watu wachache wamejitahidi sana.”
Alipotaja jina la Jamal kuwa miongoni mwa waliofaulu zaidi darasa lote lilishangaa. Jamal akamtazama Asha na kutabasamu kimya kimya.
Aliporudi nyumbani jioni aligundua jambo moja muhimu wakati mwingine msaada mdogo kutoka kwa rafiki unaweza kubadilisha kabisa siku mbaya kuwa mwanzo wa mafanikio.
emakulatemsafiri@gmail.com
0653903872



Post a Comment