USIMHUKUMU MTU KWA MUONEKANO

 


Emakulata Msafiri

Mwanakwetukids

Asubuhi yenye pilikapilika mjini magari yakipiga honi na watu wakikimbizana na shughuli zao aliishi mvulana mmoja aitwaye Kelvin. Kelvin alipenda sana kuonekana nadhifu na alikuwa akichagua marafiki kulingana na mavazi yao.

Siku moja mwanafunzi mpya alikuja shuleni kwao jijini. Jina lake lilikuwa Elika. Alivaa sare iliyochakaa kidogo na begi lake lilikuwa la zamani. Wanafunzi wengi walimtazama kwa mshangao wengine wakacheka kimyakimya.

Kelvin alimwangalia na kusema “Huyo haonekani kama mtu wa kucheza naye.”

Elika hakujali alikuwa mtulivu na mwenye bidii darasani. Alijibu maswali vizuri na hata kusaidia wanafunzi wengine kuelewa masomo.

Siku moja mwalimu aliwapa wanafunzi kazi ya kikundi. Kelvin alijikuta kwenye kikundi kimoja na Elika. Hakuwa na furaha lakini hakuwa na chaguo.

Walipoanza kazi Kelvin aligundua kuwa Elika alikuwa mwerevu sana. Alielezea masomo kwa urahisi hadi kila mtu akaelewa. Kikundi chao kilifanya vizuri kuliko vikundi vyote.

Baadaye walipokuwa wanarudi nyumbani Kelvin alikumbwa na tatizo aliporwa kalamu na vitabu na watoto wakorofi njiani. Alibaki amesimama bila kujua afanye nini.

Ghafla Elika alitokea. Alimsaidia Kelvin kukusanya vitu vyake na hata kumpeleka sehemu salama. Kelvin alihisi aibu. Akasema “Samahani Elika nilikuhukumu vibaya kwa muonekano wako.” Elika akatabasamu na kusema “Sio kila kinachoonekana nje kinaonesha kilicho ndani.”



Kuanzia siku hiyo Kelvin alibadilika. Alijifunza kuwa watu wanapaswa kuheshimiwa kwa tabia zao si muonekano wao. Na kila alipokutana na mtu mpya alikumbuka somo lake. Usimhukumu mtu kwa muonekano.

emakulatemsafiri@gmail.com

0653903872


0/Post a Comment/Comments