UKWELI WA MOYO HUONEKANA KUPITIA MATENDO

 


Emakulata Msafiri

Mwanakwetukids.

Mji wa Bahati aliishi kijana aitwaye Imani. Imani alikuwa kijana mwenye ndoto kubwa za kuwa tajiri na maarufu lakini alikuwa na tabia moja mbaya alipenda kujisifu na kudanganya kuhusu maisha yake.

Siku moja alisikia uvumi kuhusu kioo cha ajabu kilichokuwa kikifichwa kwenye mnara wa zamani nje ya mji. Ilisemekana kuwa kioo hicho hakiakisi sura ya nje tu bali pia kinaonesha ukweli wa moyo wa mtu.

Imani alitamani sana kukiona. “Kama nikikipata watu wote wataniheshimu zaidi” alijisemea.

Alianza safari yake kwenda kwenye mnara huo. Njiani alikuta watu wengi wakihitaji msaada mzee aliyebeba mizigo mizito, mtoto aliyepotea na mfanyabiashara aliyepoteza bidhaa zake.

Lakini Imani aliwapuuza wote. Alisema “Sina muda nina kitu kikubwa zaidi cha kufanya.”

Hatimaye alifika kwenye mnara mkubwa uliokuwa umezungukwa na ukungu mzito. Ndani kulikuwa kimya sana.

Alipopanda juu alikiona kioo kikubwa kilichong’aa ukutani.

Hatimaye alisema kwa furaha. Alisimama mbele ya kioo. Ghafla kioo kilianza kung’aa kwa nguvu na kuonyesha picha mbalimbali lakini si sura yake ya nje.

Kilionesha matukio yake yote ya ubinafsi, uongo na jinsi alivyowapuuza watu njiani.

Imani alishtuka sana. “Hii si kweli!” Kioo kilizungumza kwa sauti ya utulivu

“Huu ndio moyo wako halisi unaoonekana kwa wengine hata kama wewe hujioni hivyo.”

Imani alinyamaza. Alijiona ndani ya kioo akiwa tofauti kabisa na alivyofikiri yeye ni.

Alijisikia aibu kubwa. Aliposhuka kurudi njiani alikutana tena na wale watu aliowapuuza. Safari hii alisimama.

“Samahani… naweza kusaidia?” aliuliza kwa unyenyekevu.

Alisaidia mzee kubeba mizigo akamrudisha mtoto nyumbani na akamsaidia mfanyabiashara kukusanya bidhaa zake.

Kwa mara ya kwanza alihisi furaha ya kweli moyoni mwake. Aliporudi kwenye mnara baada ya siku kadhaa kioo kilikuwa bado pale lakini safari hii kilionesha picha tofauti mtu mnyenyekevu mwenye huruma na anayesaidia wengine.

emakulatemsafiri@gmail.com

0653903872


0/Post a Comment/Comments