Emakulata Msafiri
Mwanakwetukids
Katika kijiji kidogo kilichoitwa Upendo waliishi watoto watatu waliokuwa marafiki wa karibu sana Juma, Lina na Kito. Watoto hawa walipenda sana kusikiliza hadithi za wazee kuhusu msitu wa ajabu uliokuwa karibu na kijiji chao uliitwa Msitu wa Giza.
Ilisemekana kuwa ndani ya msitu huo kulikuwa na chemchemi ya maji ya miujiza yeyote anayekunywa maji yake hupata hekima kubwa. Lakini pia kulikuwa na onyo “Msitu huo si wa kuchezea unaweza kumpoteza mtu asiye na moyo wa subira.”
Siku moja Juma alisema “Hebu tuende tukatafute ile chemchemi!”
Lina alihofia kidogo. “Vipi tukipotea?”
Kito akasema kwa ujasiri “Tukiwa pamoja hatutapotea.” Baada ya kusita kidogo walikubaliana kwenda. Walibeba chakula kidogo, maji na fimbo za kujilinda kisha wakaingia msituni asubuhi mapema. Mwanzoni kila kitu kilionekana cha kawaida. Ndege waliimba, upepo ulivuma polepole na miti ilitoa kivuli kizuri. Lakini walipozidi kwenda ndani zaidi mwanga ulianza kupungua na sauti za ajabu zilianza kusikika.
“Umesikia hiyo?” Lina aliuliza kwa sauti ya chini. “Ndio… kama mtu anatembea nyuma yetu "Juma alisema huku akiangalia nyuma.
Lakini hawakuona mtu yeyote. Walitembea kwa muda mrefu hadi wakafika mahali ambapo njia iligawanyika mara tatu.
“Sasa tufanyeje?” Kito aliuliza.
Juma alisema “Tuchague njia ya kushoto.” Lina akasema “Hapana nadhani ya kulia inaonekana salama zaidi.” Wakabishana kwa muda mpaka wakasikia sauti ya mzee ikisema “Msiwe na haraka… sikilizeni mioyo yenu.”Waligeuka lakini hawakuona mtu. “Labda ni uchawi wa msitu huu” Lina alisema.
Hatimaye waliamua kukaa chini kidogo na kufikiri kwa utulivu. Baada ya muda Kito alisema “Hebu tuchague njia ya katikati inaonekana haijaguswa sana.”
Wote walikubaliana.Walipoanza kutembea njia hiyo ghafla waliona mwanga mdogo ukiangaza mbele yao. Walikimbia kuelekea kule na wakakuta chemchemi ndogo yenye maji safi sana yanayong’aa kama kioo.“Tumeipata!” Juma alipiga kelele kwa furaha.
Kabla hawajanywa maji sauti ile ile ilirudi: “Maji haya si ya kila mtu. Ni ya wale walioweza kuwa wavumilivu na kushirikiana.”Watoto walitazamana. Walikumbuka jinsi walivyobishana lakini pia jinsi walivyokaa pamoja na kufanya uamuzi kwa utulivu. Kila mmoja alikunywa maji kidogo.
Ghafla walihisi kama akili zao zimekuwa wazi zaidi. Walianza kuelewa mambo kwa haraka na hata njia ya kurudi nyumbani ilionekana wazi kabisa.
Walirudi kijijini salama.Kuanzia siku hiyo, Juma, Lina na Kito walikuwa watoto wenye hekima na walisaidia wengine kijijini kwa mawazo yao mazuri.
emakulatemsafiri@gmail.com
0653903872



Post a Comment