Emakulata Msafiri
Mwanakwetukids.
Katika kijiji kilichozungukwa na milima ya kijani aliishi msichana mdogo aitwaye Saida. Saida alikuwa mchangamfu sana lakini alikuwa na tabia moja mbaya alipenda kusema maneno makali akiwa na hasira. Kila alipogombana na wenzake alikuwa akisema maneno kama “Wewe huwezi kitu!” au “Huna akili!” Baada ya kusema alijuta lakini maneno tayari yalikuwa yametoka. Siku moja alipokuwa akichunga mbuzi karibu na mlima aliona kitu cha ajabu kilichong’aa chini ya mti mkubwa. Ilikuwa jiwe dogo la rangi ya bluu liking’aa kama nyota.
Alipoligusa ghafla upepo ulivuma na sauti ya ajabu ikasema“Mimi ni Jiwe la Maneno. Kila neno unalosema nitalihifadhi.”Saida aliogopa kidogo. “Unaweza kuongea?!”Jiwe likasema “Siyo mimi kuongea tu… bali nitakuonyesha uzito wa maneno yako.”Saida hakuelewa lakini alienda nyumbani nalo. Siku iliyofuata aligombana na rafiki yake Halima. Kwa hasira akasema “Wewe ni mpumbavu!” Ghafla jiwe likang’aa kwa nguvu.
Halima aliondoka akiwa na huzuni kubwa.Usiku ule Saida aliota ndoto ya ajabu. Aliona kila neno baya alilosema likibadilika kuwa mawe makubwa na kuangukia watu aliowaumiza. Watu walikuwa wakitembea kwa shida kwa sababu ya mizigo ya maneno yake.
Alipoamka alilia. “Sikutaka kuwaumiza…”
Jiwe likamwambia “Maneno yana uzito kuliko unavyofikiri. Hayawezi kurudi nyuma yakishatoka.” Kuanzia siku hiyo Saida alijitahidi sana kubadilika. Alianza kufikiri kabla ya kuongea. Alisema maneno mazuri kama “Samahani, Asante na “Unaweza.”
Polepole aliona mabadiliko marafiki zake walimkaribia tena na watu walifurahi kuwa karibu naye. Lakini wakati mwingine alipokasirika jiwe lilitoa mwanga mdogo kama ukumbusho. Siku moja alimuona Halima akiwa mgonjwa. Saida alimwendea na kusema kwa upole
“Samahani kwa yale niliyosema zamani nimejifunza.” Halima alitabasamu kwa uchovu na kusema “Nimekusamehe.”Ghafla jiwe lilianza kung’aa sana kisha likapotea polepole hewani.
Saida alishangaa. “Limeenda wapi?”Sauti ya jiwe ilisikika mbali “Limekuwa ndani ya moyo wako sasa unalinda maneno yako mwenyewe.” Kuanzia siku hiyo Saida alikua msichana mwenye hekima anayechagua maneno yake kwa uangalifu.
emakulatemsafiri@gmail.com
0653903872



Post a Comment