Emakulata Msafiri
Mwanakwetukids
Hapo zamani za kale katika ufalme mkubwa ulioitwa Amani aliishi mfalme mwenye haki pamoja na binti yake aitwaye Zahra. Zahra alikuwa mrembo na mwenye akili lakini alikuwa na tatizo moja alipenda kuhukumu watu kwa muonekano wao.
Siku moja mfalme aliugua sana. Waganga walijaribu kila dawa lakini hawakufaulu.
Mzee mmoja mwenye hekima alifika ikulu na kusema
“Mfalme anaweza kupona lakini kuna sharti moja lazima upate maji kutoka kwenye Chemchemi ya Ukweli iliyoko mbali sana msituni.”
Zahra alijitolea kwenda. “Nitakwenda kumuokoa baba yangu.”
Alivalia mavazi ya kifalme na kuchukua walinzi wachache wakaanza safari ndefu. Njiani walikutana na mzee maskini aliyevaa nguo zilizochakaa. Alisema
“Tafadhali naomba maji kidogo.”
Zahra alimtazama kwa dharau. “Hatuna muda wa kusimama kwa kila mtu.”
Wakaendelea na safari.
Baadaye, walikutana na mtoto mdogo aliyepotea. Alilia na kusema “Nisaidieni nirudi nyumbani.”
Zahra akasema “Hatuwezi kuchelewa kwa sababu yako.”
Walipofika kwenye msitu ule mkubwa walipoteza njia. Walizunguka sana bila mafanikio.
Hatimaye walirudi pale pale walipoanzia karibu na yule mzee maskini.
Mzee akasema kwa hekima “Njia ya Chemchemi ya Ukweli haionekani kwa macho bali kwa moyo.” Zahra alinyamaza. Alikumbuka jinsi alivyowapuuza watu aliokutana nao.
Kwa sauti ya unyenyekevu alisema “Nisamehe. Nilifanya makosa.”
Mzee alitabasamu. Ghafla akabadilika kuwa mtu mwenye mwanga mkubwa usoni.
“Mimi ndiye mlinzi wa chemchemi" alisema.
Zahra alishangaa sana.Mzee alimpa pete ndogo ya kung’aa. “Pete hii itakuongoza, lakini tu ikiwa moyo wako ni wa huruma.”
Safari hii Zahra aliamua kubadilika. Alipokutana tena na yule mtoto mdogo alimsaidia kumrudisha nyumbani. Alipokutana na watu wengine njiani aliwasaidia bila kusita.
Kila alipofanya wema pete ile iling’aa zaidi.Hatimaye pete ilimwongoza hadi kwenye chemchemi ya maji safi kabisa. Alichota maji na kurudi haraka ikulu.
Alipompa baba yake maji yale mfalme alipona polepole hadi akasimama tena.
Ufalme wote ulifurahi. Zahra alijifunza somo kubwa. Alianza kuwaheshimu watu wote bila kujali muonekano wao.Mfalme alisema kwa furaha
“Umeokoa maisha yangu lakini zaidi ya yote umeokoa moyo wako.”
emakulatemsafiri@gmail.com
0653903872



Post a Comment