PENDA NA TUNZA MAZINGIRA


Emakulata Msafiri

Mwanakwetukids

Lulu alikuwa mtoto mchangamfu aliyesoma darasa la pili. Alipenda sana mazingira safi na maua mazuri. Kila asubuhi Lulu alikuwa anafika shule mapema kuliko wanafunzi wengine.

Siku moja Lulu aliona kwamba maua ya bustani ya shule yalikuwa yanaanza kunyauka kwa sababu hakuna aliyekuwa anayemwagilia maji. Majani ya maua yalikuwa yamepoteza rangi yake ya kijani na baadhi ya maua yalikuwa yameinama chini.

Lulu alisikitika sana. Akaamua kufanya jambo.

Baada ya shule Lulu alimwambia mwalimu wake “Mwalimu naomba niwe namwagilia maua ya shule kila asubuhi kabla ya darasa kuanza.”

Mwalimu alitabasamu na kusema“Hilo ni wazo zuri sana Lulu. Endelea.”

Kuanzia siku iliyofuata Lulu alikuwa anaamka mapema. Alibeba ndoo ndogo ya maji kutoka kwenye bomba la shule na kumwagilia maua taratibu. Alikuwa anahakikisha maji yanafika kwenye mizizi ya maua bila kuharibu miche midogo.

Baada ya wiki mbili wanafunzi na walimu walianza kuona mabadiliko. Maua yalichanua vizuri na bustani ya shule ilionekana nzuri zaidi. Nyuki wadogo na vipepeo walikuwa wanaruka juu ya maua yenye rangi angavu.

Wanafunzi wengine walipenda kazi ya Lulu. Wakaamua pia kusaidia kutunza mazingira ya shule. Wengine walikuwa wanakusanya takataka uwanjani na wengine walisaidia kumwagilia maua.

Siku ya mkutano wa shule mwalimu alisimama mbele ya wanafunzi na kusema

“Nataka nimshukuru Lulu kwa upendo wake kwa mazingira. Kitendo chake kimetufundisha umuhimu wa kutunza vitu vya shule.”



Wanafunzi wote walimpigia Lulu makofi. Lulu alifurahi lakini hakujivunia. Alijua kwamba alifanya jambo jema kwa moyo wake. Baada ya muda shule yao ikawa maarufu kwa kuwa na bustani nzuri ya maua.

emakulatemsafiri@gmail.com

0653903872



0/Post a Comment/Comments