LOVE NA BUSTANI YA MAMA

Emakulata Msafiri

Mwanakwetukids

Love alikuwa msichana mdogo aliyeishi na mama yake kijijini. Mama yake alikuwa mkulima na alikuwa na bustani ndogo nyuma ya nyumba yao.

Katika bustani hiyo kulikuwa na mboga za majani, nyanya na maua mazuri ya alizeti. Mama alikuwa akisema. “Bustani hii ni kama familia yetu inahitaji huduma na upendo.”

Love alipenda kusaidia mama yake ingawa wakati mwingine alitamani kucheza na marafiki zake. Kila siku baada ya kurudi shule Love alibeba ndoo ya maji na kumwagilia mimea bustanini.

Siku moja Love alichoka kidogo na kusema

“Mama kwa nini tunafanya kazi nyingi hivi? Si tunaweza kupumzika?”

Mama alikaa karibu naye na kusema “Mmea unaoachwa bila maji hufa. Vivyo hivyo maisha yanahitaji juhudi na uvumilivu.”

Love hakuelewa vizuri wakati huo lakini aliendelea kusaidia.

Miezi ilipita na bustani ya mama ilikua nzuri sana. Mboga ziliongezeka na maua yalichanua kwa rangi nzuri. Watu wa kijijini walikuja kununua mboga kutoka kwa mama wa Love.

Mama alipata pesa kidogo za kuendesha maisha na kununua vitu vya shule vya Love.

Siku moja Love alishangaa kuona mama amemnunulia jozi mpya ya viatu vya shule. Alifurahi sana na kumkumbatia mama yake.

Mama alimwambia “Hii ni zawadi kwa sababu ya msaada wako na uvumilivu wako.”

Love alitabasamu na kuelewa kwamba kazi yake ndogo ilikuwa na matokeo makubwa.


emakulatemsafiri@gmail.com

0653903872




0/Post a Comment/Comments