MTOTO ALIYEPENDA TUNDA LA CHENZA

 

Emakulata Msafiri

Mwanakwetukids

Watoto walipenda maembe na mapapai lakini mtoto mmoja aliyeitwa Baraka alipenda sana tunda la chenza. Kila siku baada ya shule alipitia njia ndefu ili tu afike kwenye mti mmoja mkubwa uliokuwa kandokando ya shamba la babu Juma.

Babu Juma alikuwa mkulima mwenye bidii. Aliwaambia watoto wote “Msipande mti bila ruhusa matawi yake ni dhaifu.” Watoto wengi walitii lakini Baraka alishindwa kujizuia. Alitamani sana yale matunda yaliyong’aa juu kabisa ya mti.

Siku moja alifika mapema kabla ya mtu yeyote. Akaangalia huku na huku kisha akaanza kupanda polepole. Alipofika juu alifikia tunda kubwa kuliko yote. Alipolivuta tawi likavunjika ghafla.

Baraka akaanguka kwenye majani. Hakuumia sana lakini aliogopa sana. Babu Juma alisikia kishindo na akakimbia hadi pale. Badala ya kumpiga kelele alimnyanyua na kumuuliza “Umejifunza nini leo?”

Baraka alinyamaza kisha akasema “Ningengoja unipe nisingeumia wala kuvunja mti.”

Babu Juma akatabasamu. Akaokota matunda yaliyoiva na kumpa kikapu kidogo. “Matunda matamu yanahitaji subira” alimwambia.

Tangu siku hiyo Baraka alisaidia kumwagilia miti kila jioni. Alijifunza kutunza kabla ya kuvuna. Na ajabu ni kwamba alianza kufurahia zaidi kula matunda aliyoyatunza mwenyewe kuliko yale aliyoyaiba.

emakulatemsafiri@gmail.com

0653903872


0/Post a Comment/Comments