MALEZI MEMA HUANZA TANGU UTOTONI

 

Emakulata Msafiri

Mwanakwetukids

Kulipopambazuka alfajiri ukungu mwepesi ulitanda juu ya paa za nyumba za udongo na jogoo akawika kuashiria mwanzo wa siku mpya. Upepo mwanana ulivuma taratibu ukibeba harufu ya ardhi iliyonea umande wa usiku.

Kulikua na mama mmoja aitwaye Asha pamoja na mwanawe Aika. Maisha yao hayakuwa ya anasa lakini yalijaa upendo na mshikamano.

Kila siku mama Aika aliamka mapema kwenda kuchota maji mtoni uliokuwa mbali kidogo na nyumbani kwao. Siku moja alipoona mama yake akijiandaa kubeba ndoo alimwambia kwa sauti ya upole

“Mama leo naomba nije nikusaidie.”Mama yake alitabasamu macho yake yakijaa furaha.

“Karibu mwanangun” akasema “kazi ni wajibu wetu sote.”

Walitembea pamoja kwenye njia nyembamba ya vumbi.Aika alibeba ndoo ndogo akijitahidi kulingana na hatua za mama yake. Walipofika mtoni mama yake alimfundisha kwa utulivu jinsi ya kushika ndoo vizuri na kuchota maji bila kuyamwaga.

Aika alijaribu mara ya kwanza maji yakamwagika kidogo. Hakukata tamaa. Alijaribu tena safari hii akafanikiwa. Mama yake alimpongeza kwa maneno ya kumtia moyo.

Waliporudi nyumbani alihisi uchovu mikononi lakini moyo wake ulikuwa mwepesi kwa furaha. Kuanzia siku hiyo akawa anamsaidia mama yake si tu kuchota maji bali pia kufagia na kufanya kazi nyingine za nyumbani.Majirani walipomwona walimsifu mama yake wakisema.

“Kweli mtoto mleavyo ndivyo akuavyo.”Aika alikua mtoto mwenye bidii, heshima na moyo wa kusaidia wengine kwa sababu alifundishwa mapema thamani ya kazi na upendo.

emakulatemsafiri@gmail.com

0753903872


0/Post a Comment/Comments