THAMINI HATA KIDOGO ULICHONACHO

Emakulata Msafiri

Mwanakwetukids

Amani alikuwa mwanafunzi wa darasa la nne. Aliishi na mama yake katika nyumba ndogo ya kupanga karibu na shule.

Kila siku alikuwa anaenda shule kwa miguu. Viatu vyake vilikuwa vimechakaa sana mbele vilikuwa vimepasuka kidogo. Wakati mvua ikinyesha miguu yake ilikuwa inalowa.

Wanafunzi wengine walikuwa wanamcheka. “Sasa Amani hivyo viatu au midomo ya samaki?” walitania.Amani aliumia moyoni lakini hakujibu. Mama yake alikuwa anafanya kazi ya kufua nguo za watu hivyo pesa ilikuwa haitoshi haraka.

Siku moja mwalimu aliwaambia “Wiki ijayo tutakuwa na gwaride la shule. Kila mwanafunzi aje nadhifu.”Amani alinyamaza. Alijua hatapata viatu vipya mapema.

Jioni ile alimkuta mama amechoka sana. Mikono ilikuwa imevimba kwa sabuni. Amani akaamua kitu kimya kimya.

Baada ya kazi za nyumbani alichukua sindano na uzi. Akaosha viatu vyake vizuri akavikausha kisha akaanza kushona polepole pale palipopasuka.

Ilichukua muda mrefu. Vidole vilimuuma Lakini aliendelea.

Asubuhi yake alivaa sare yake safi na viatu alivyovishona. Havikuwa vipya lakini vilionekana nadhifu.Shuleni mwalimu alipita akakagua wanafunzi. Aliposimama kwa Amani alitabasamu.

“Hivi viatu si vipya… lakini vimetunzwa vizuri sana. Nani kakusaidia?”

Amani akasema kwa aibu “Mimi mwenyewe mwalimu.”

Mwalimu akamshika begani “Huu ndio uwajibikaji Unajali ulicho nacho.”

Siku hiyo hakupata tu pongezi alichaguliwa kuwa kiongozi wa darasa.

Jioni alipomwambia mama macho ya mama yalijaa machozi ya furaha.

emakulatemsafiri@gmail.com

0653903872


0/Post a Comment/Comments