Emakulata Msafiri
Mwanakwetukids
Asha alikuwa mwanafunzi wa darasa la nne katika Shule ya Msingi Mwanga. Alikuwa mtoto mtiifu na alipenda kusoma hasa somo la Kiswahili. Kila jioni aliporudi nyumbani alikuwa akifanya kazi zake za shule kabla ya kucheza na marafiki zake.
Siku moja jioni baada ya kurudi kutoka shuleni Asha alifungua begi lake ili kufanya kazi ya hesabu. Alishtuka kuona daftari lake la hesabu halikuwepo. Alilitafuta chini ya kitanda, mezani na hata jikoni lakini halikupatikana. Moyo wake ulijaa hofu kwa sababu mwalimu alikuwa amesema kesho atapitia daftari zote.
Usiku huo Asha hakulala vizuri. Asubuhi alipofika shuleni alikuwa na huzuni. Akiwa darasani alimwona rafiki yake Neema amekaa kimya na hakucheza na watoto wengine kama kawaida. Wakati wa mapumziko Asha alimkaribia Neema na kumuuliza kama ana tatizo.
Kwa sauti ya aibu Neema akasema “Asha jana nilichukua begi lako kwa bahati mbaya. Ndani yake kulikuwa na daftari lako la hesabu. Nilihofia kukuambia.”
Asha alihisi huzuni kidogo lakini alikumbuka mafunzo ya wazazi wake kuhusu kusamehe. Akamwambia Neema.
“Asante kwa kusema ukweli. Kila mtu hukosea.”
Neema akamrudishia daftari hilo na akaomba msamaha. Wote wawili wakaingia darasani wakiwa na furaha. Mwalimu alipokagua daftari Asha alipongezwa kwa kazi nzuri.
emakulatemsafiri@gmail.com
0653903872



Post a Comment