MTOTO ALIYETAKA KUWA BABA LAKINI AKASHINDWA!


Na, Emakulata Msafiri

Siku moja katika kijiji kidogo cha Mbopo, waliishi Kibaba (jina lake Mussa), Kimama (anaitwa Asha), na mtoto wao mdogo aitwaye Juma. Walikuwa familia ya kawaida sana, lakini walipendana mno.

Asubuhi moja, Kibaba aliamka mapema sana kwenda kazini. Akamwambia Kimama:

"Asha mpenzi, naenda kazini. Usisahau kupika ugali wa muhogo kwa chakula cha mchana."

Kimama akaitikia kwa upole:

"Usijali mume wangu. Nitahakikisha kila kitu kiko tayari ukirudi."

Baada ya Kibaba kuondoka, Kimama akaanza kusafisha nyumba, huku mtoto Juma akiwa anacheza na mchanga nje. Lakini Juma hakuwa msikivu siku hiyo. Alikataa kuoga, akakataa kula, na hata alipoulizwa aende dukani kununua chumvi, alikataa kabisa.

Kimama akamuita:

"Juma, njoo hapa! Kwa nini hutaki kuniita mama leo?"

Juma akajibu kwa kiburi:

"Leo mimi ni baba! Sitaki kuitwa mtoto!"

Kimama akashangaa lakini akamcheka tu. Akasema:

"Basi kama wewe ni baba, pika ugali, fanya usafi, na ulale kitandani peke yako!"

Juma akashindwa kabisa, akarudi haraka kwa mama yake akasema:

"Samahani mama. Nataka niwe mtoto tena. Naomba chakula."

Kimama akamkumbatia, akampatia chakula, kisha wakakaa wote kusubiri Kibaba arudi. Jioni ilipofika, Kibaba akarudi na zawadi ya pipi kwa Juma.

Wote wakakaa mezani kula ugali wa muhogo kwa furaha.


emakulatemsafiri@gmail.com

0653903872


0/Post a Comment/Comments