BARUA ZA ZAMANI ZILIZOFICHUA HISTORIA YA ABBASI KANDORO

 



Adeladius Makwega


Ofisi ya Rais, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Dodoma

 

Oktoba 12, 2026, Mwanakwetu alitamani kuandika makala kuhusu maisha na mchango wa marehemu Profesa Geoffrey Mmari, aliyefariki dunia Oktoba 11, 2026. Profesa Mmari aliwahi kushika nyadhifa mbalimbali za uongozi katika taasisi za elimu ya juu nchini, zikiwamo Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kuanzia mwaka 1984 hadi 1988, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kuanzia mwaka 1988 hadi 1991, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) kuanzia mwaka 1993 hadi 2005, na taasisi nyingine kuanzia mwaka 2005 hadi 2013, kama inavyothibitishwa na kumbukumbu rasmi.

 

Katika maandalizi ya makala hiyo, Mwanakwetu aliona umuhimu wa kurejea nyaraka za kihistoria ili kupata ushahidi wa maandishi kuhusu maisha na utumishi wa watu waliochangia maendeleo ya taifa.

 

Hivyo, aliwasiliana na maafisa wa Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa katika ofisi za Dar es Salaam na Dodoma kwa lengo la kutafuta nyaraka za zamani zinazoweza kusaidia kuijenga upya historia ya watumishi wa umma.

 

Miongoni mwa nyaraka alizokuwa akitafuta ni barua ya maombi ya kazi ya ualimu iliyoandikwa na Profesa Mmari mwaka 1955, inayohusishwa na kazi ya ualimu huko Bukoba.

 

Nyaraka za aina hii zina umuhimu mkubwa kwa sababu hutuwezesha kuelewa safari za maisha, elimu, ajira na maendeleo ya kitaaluma ya watu waliochangia katika kujenga jamii na taifa.

Katika juhudi hizo, Mwanakwetu alikutana na maafisa mbalimbali waliotoa msaada katika kufuatilia kumbukumbu husika. Miongoni mwao alikuwa Lear Clara Ngairo, Afisa Kumbukumbu katika ofisi ya Dodoma.

 

Wakati wa kufanya utafiti huo, Mwanakwetu alikutana pia na nyaraka kadhaa zinazomhusu A. H. Kandoro. Nyaraka hizi zilivutia kwa namna zinavyotoa mwanga kuhusu masuala ya ajira, elimu, taaluma na mabadiliko ya kiutumishi katika Serikali ya Tanzania.

 

Miongoni mwa nyaraka hizo ni barua ya tarehe 17 Desemba 1980, ambayo A. H. Kandoro aliandika kwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, akiomba kuhamia Idara ya Serikali za Miji.

 

Barua hiyo, yenye mada “Kuhamia Idara ya Miji”, inaonyesha kuwa Kandoro alikuwa akitafuta nafasi ya kutumia elimu na uzoefu wake wa uchumi katika eneo jingine la utumishi wa umma.

 

Katika barua yake, Kandoro alieleza kuwa alikuwa mchumi katika idara yake tangu mwaka 1976. Alibainisha pia kuwa alikuwa amepata shahada ya kwanza ya Uchumi (B.A. Economics) mwaka 1976 na shahada ya uzamili ya Uchumi (M.A. Economics) mwaka 1980 kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Kwa kuzingatia elimu na uzoefu wake, Kandoro aliona kuwa angeweza kutumia ujuzi wake wa kitaaluma kwa manufaa zaidi katika Idara ya Serikali za Miji. Aliwasilisha ombi lake rasmi na kuambatanisha vyeti vya elimu,na wasifu wake ili kusaidia mamlaka husika kufanya uamuzi.

 

Ushahidi mwingine muhimu unaonekana katika barua ya tarehe 5 Januari 1981 kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu. Barua hiyo inarejelea ombi la Kandoro la tarehe 17 Desemba 1980 na kumjulisha kuwa ombi lake la kuhamia Idara ya Serikali za Miji limekubaliwa.

 

Katika barua hiyo, Mkurugenzi wa Mashirika katika Ofisi ya Waziri Mkuu aliombwa kumruhusu Kandoro kujiunga na Idara ya Serikali za Miji.

 

Kwa hiyo, barua hizo mbili zinaonyesha hatua mbili muhimu katika mchakato huo: kwanza, Kandoro kuwasilisha ombi lake la uhamisho; na pili, Serikali kutoa taarifa kwamba ombi hilo limekubaliwa.

 

Huu ni mfano mzuri wa namna nyaraka za kiutumishi zinavyoweza kusaidia kufuatilia maamuzi ya Serikali na mabadiliko katika maisha ya watumishi wake.

Katika utafiti wa kihistoria, si maandishi makuu pekee yanayoweza kuwa na taarifa muhimu. Mihuri, sahihi, tarehe, kumbukumbu za kupokelewa na maelezo ya pembeni vinaweza kusaidia kuelewa namna nyaraka zilivyopokelewa, kushughulikiwa na kutumika katika maamuzi ya kiutawala.

 

A. H. Kandoro anakumbukwa kwa utumishi wake katika uongozi wa umma, ikiwa ni pamoja na kushika nafasi za Mkuu wa Wilaya na Mkuu wa Mkoa katika maeneo mbalimbali nchini. Taarifa za wasifu wake zinaeleza kuwa aliwahi kuhudumu katika mikoa ya Tabora, Arusha, Dar es Salaam, Mwanza na Mbeya, ambako alistaafu akiwa Mkuu wa Mkoa.

Taarifa nyingine za wasifu wake zinaeleza kuwa alizaliwa tarehe 9 Septemba 1950 katika kijiji cha Ihemi, Kata ya Mgamo, Wilaya ya Iringa Vijijini, na alifariki dunia usiku wa kuamkia tarehe 28 Aprili 2018 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam.

 Nyaraka za aina hii zina umuhimu kwa watafiti, wanahistoria, wanafunzi na wananchi wanaotaka kuelewa historia ya utumishi wa umma nchini Tanzania. Zinaweza kusaidia kujibu maswali kuhusu elimu ya viongozi, safari zao za kikazi, maamuzi ya kiutawala na namna taasisi za Serikali zilivyofanya kazi katika vipindi tofauti.

Safari ya Mwanakwetu ya kutafuta nyaraka zinazohusu Profesa Geoffrey Mmari ilimfungulia pia mlango wa kukutana na kumbukumbu za A. H. Kandoro. Tukio hili linatukumbusha kuwa utafiti wa kihistoria unaweza kuibua taarifa nyingine muhimu ambazo, kwa namna moja au nyingine, zinasaidia kuhifadhi na kuandika historia ya taifa.

Barua ya Kandoro ya mwaka 1980 na majibu ya Serikali ya Januari 1981 si karatasi za zamani tu. Ni ushahidi wa maandishi unaotusaidia kuelewa namna watumishi wa umma walivyotumia elimu na utaalamu wao kutafuta nafasi za kuchangia maendeleo ya nchi.

Kwa maana hiyo, Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa ni zaidi ya mahali pa kuhifadhi mafaili. Ni hazina inayolinda kumbukumbu za taifa, kusaidia utafiti na kuhakikisha kuwa vizazi vya sasa na vijavyo vinapata nafasi ya kujifunza kutokana na historia.

Mwanakwetu yupo, akiendelea kutafuta, kusoma na kusimulia historia iliyohifadhiwa ndani ya nyaraka za taifa.

 

Kwa mawasiliano: makwadeladius@gmail.com | 0717 649 257













 



 

 

 

 

0/Post a Comment/Comments