Emakulata Msafiri
Mwanakwetukids
Wakati wa mapumziko shuleni wanafunzi walipenda kucheza pamoja na kushirikishana vitafunwa. Hata hivyo kulikuwa na mtoto mmoja ambaye kila mara alitaka mambo yafanyike kwa njia yake.
Walipoamua kucheza mpira alitaka awe ndiye anayeamua timu. Walipogawana vitafunwa alichukua sehemu kubwa na alipokosolewa alikasirika na kuondoka.
Kadiri siku zilivyopita wenzake walianza kumuepuka. Mwanzoni alidhani walikuwa na wivu naye lakini alipoona hata rafiki yake wa karibu akichagua kucheza na wengine alianza kujiuliza kwa nini alikuwa akiachwa peke yake.
Siku moja mwalimu aliwapa wanafunzi kazi ya kufanya kwa vikundi. Hakuna aliyekuwa tayari kujiunga naye. Alijisikia vibaya na ndipo alipogundua kuwa tabia yake ilikuwa imewaumiza wenzake.
Baada ya kipindi alimwomba mwalimu ushauri. Alielekezwa umuhimu wa kusikiliza wengine, kushirikiana na kukubali kuwa kila mtu ana haki ya kutoa maoni yake.
Alianza kubadilika kwa vitendo akijifunza kugawana na kuomba msamaha anapokosea polepole wenzake walianza kumwamini tena.
emakulatemsafiri@gmail.com
0653903872


Post a Comment