WEMA HAUHITAJI UTAJIRI UNAHITAJI MOYO WA HURUMA

 

Emakulata Msafiri 

Mwanakwetukids.

Kila asubuhi mtoto mmoja alikuwa akitembea kwa miguu kwenda shule. Njiani alipita sehemu yenye mawe na matope hivyo viatu vyake vilichafuka kila siku. Wakati mwingine alitamani angeacha kabisa kuvaa viatu hivyo kwa sababu vilionekana vimechakaa.

Siku moja alipofika shuleni alimwona mwanafunzi mwenzake akiwa amekaa pembeni ya darasa. Alikuwa hana viatu kabisa. Miguu yake ilikuwa imejaa michubuko kutokana na kutembea kwenye mawe.

Baada ya masomo yule mtoto alifika nyumbani na kumwambia baba yake kuhusu rafiki yake. Baba yake alimwambia "Kama una kitu unachoweza kushiriki na mwingine usisite kufanya hivyo".

Siku iliyofuata walinunua jozi mpya ya viatu. Badala ya kuhifadhi viatu vyake vya zamani aliviosha vizuri akavipangusa na akampa yule rafiki yake.

Furaha iliyoonekana usoni mwa rafiki yake ilikuwa kubwa kuliko alivyotarajia. Tangu siku hiyo wote wawili walikuwa wakitembea kwenda shule pamoja wakiwa na tabasamu.

Mtoto huyo alitambua kuwa kutoa si lazima uwe tajiri. Wakati mwingine kitu kidogo unachokiona hakina thamani kinaweza kuwa msaada mkubwa kwa mtu mwingine.


emakulatemsafiri@gmail.com 

0653903872



0/Post a Comment/Comments