USIDHARAU KIDOGO ULICHONACHO KINAWEZA KUBADILISHA MAISHA YA MWINGINE

Emakulata Msafiri 

Mwanakwetukids

Kulikuwa na mtoto aliyependa sana kusoma lakini familia yake haikuwa na uwezo wa kununua vifaa vya kutosha vya shule. Alikuwa amebakiza daftari moja tu na kila ukurasa aliutumia kwa uangalifu mkubwa.

Siku moja akiwa darasani alimwona mwanafunzi mwenzake akilia kwa sababu hakuwa na daftari la kuandikia. Bila kusita alimchania nusu ya daftari lake na kumpa.

Mwanzoni aliogopa kwamba hataweza kumaliza muhula kwa daftari lililobaki. Hata hivyo mwalimu aliona kitendo chake na akauliza kilichotokea.

Baada ya kusikia ukweli mwalimu aliwaeleza wanafunzi umuhimu wa kushirikiana na kusaidiana. Siku iliyofuata wanafunzi na wazazi walikusanya madaftari kalamu na penseli kwa ajili ya watoto waliokuwa na uhitaji.

Mtoto aliyetoa nusu ya daftari lake alipokea daftari jipya pamoja na vifaa vingine vya shule. Lakini kilichomfurahisha zaidi si zawadi aliyopata baali kuona rafiki yake akiendelea na masomo bila kukosa.

Tangu siku hiyo darasa lao lilijulikana kwa mshikamano na upendo. Hakukuwa na mwanafunzi aliyebaki nyuma kwa sababu ya kukosa vifaa vya kujifunzia.


emakulatemsafiri@gmail.com 

0653903872



0/Post a Comment/Comments