Emakulata Msafiri
Mwanakwetukids.
Kulikuwa na ukimya mkubwa katika uwanja wa shule. Wanafunzi wote walikuwa wametulia wakisubiri kusikia sauti ya mtoto mmoja ambaye alikuwa hajawahi kupanda jukwaani hapo kabla. Ghafla, mtoto huyo alifungua mdomo wake na kuanza kuimba… sauti yake ilifanya kila mtu ageuke na kutazamana kwa mshangao.
Mtoto huyo aliitwa Amani. Tangu akiwa mdogo alikuwa na kipaji cha kuimba na kusimulia hadithi kupitia nyimbo. Alikuwa akitunga nyimbo zake mwenyewe na kuzitumia kuelezea mambo aliyoyaona katika maisha yake, kama upendo, urafiki na ndoto za watoto.
Kila jioni baada ya masomo watoto wa mtaa walikusanyika kumsikiliza Amani alipokuwa akiimba hadithi za kuvutia. Alikuwa akiimba kuhusu sungura mwenye moyo wa kusaidia, mtoto aliyependa kusoma na familia iliyoshirikiana kwa upendo.
Siku moja mwalimu wao alitangaza kuwa kungekuwa na maonesho ya vipaji shuleni. Wanafunzi wengi waliogopa kushiriki akini Amani aliamua kuonesha kipaji chake. Alipofika kwenye jukwaa alianza kuimba hadithi kuhusu mtoto aliyekuwa na ndoto kubwa licha ya changamoto alizokutana nazo.
Baada ya wimbo wake kumalizika ukumbi ulilipuka kwa makofi na vigelegele. Walimu na wazazi walifurahi kuona mtoto huyo akitumia kipaji chake kuhamasisha wengine.
Kuanzia siku hiyo Amani alijulikana kama mtoto mwenye sauti ya pekee. Aliendelea kuimba, kutunga hadithi na kuwapa watoto wengine ujasiri wa kuamini vipaji vyao.
emakulatemsafiri@gmail.com
0653903872



Post a Comment