Emakulata Msafiri
Mwanakwetukids
Pusi alikuwa paka wa mitaani jijini Dar es Salaam. Maisha yake yalikuwa ya kutafuta mabaki ya chakula sokoni au kwenye migahawa. Ata hivyo alipenda sana kushinda karibu na duka la ufundi cherehani la Mama Amina mwanamke mkarimu aliyempa chakula mara kwa mara.
Siku moja mtoto wa Mama Amina mwenye umri wa miaka mitano aliyeitwa Baraka alikuwa akicheza nje na mpira. Kwa bahati mbaya mpira uliingia kwenye mtaro mkubwa wa maji machafu kando ya barabara. Baraka alipoinama kuifikia aliteleza kwenye mwani na kutumbukia mguu mmoja ndani ya maji yaliyokuwa yakienda kasi. Alishtuka na kuanza kulia akishindwa kujivuta juu.
Ndani ya duka mama Amina hakusikia chochote kwa sababu ya kelele za cherehani.
Pusi aliona hatari hiyo. Alikimbia haraka hadi ndani ya duka na kuanza kulia kwa sauti kubwa ya ajabu: "Miao! Miao!" huku akijigongesha kwenye miguu ya Mama Amina na kukimbilia mlangoni.
Mama Amina alishangaa na kuamua kumfuata yule paka nje. Alipotoka tu alimwona mwanawe aking'ang'ania ukingo wa mtaro huku akizama. Alipiga yowe akakimbia na kumvuta Baraka juu salama.
Baada ya mshtuko kuisha Mama Amina alimwombea Pusi bakuli kubwa la maziwa na samaki wa kukaanga. Tangu siku hiyo Pusi hakuwa tena paka wa mitaani alipata makazi rasmi na familia iliyomshukuru maisha yake yote.
emakulatemsafiri@gmail.com
0653903872



Post a Comment